Mwombolezaji afariki dunia kwenye msiba wa mwanafunzi wa IFM, Kilimanjaro
Leah Ngowi enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Mei 7, 2026, wakati baadhi ya waombolezaji wakiwa katika mkesha wa msiba huo kijijini Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, mkoani Kilimanjaro.
Moshi. Mwombolezaji Leah Ngowi, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60 mkazi wa Kiboriloni wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, amefariki dunia akiwa kwenye msiba wa aliyekuwa mwanafunzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba (24).
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Mei 7, 2026, wakati baadhi ya waombolezaji wakiwa katika mkesha wa msiba huo kijijini Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumzia tukio hilo, shangazi wa marehemu, Ruth Fabian amesema walikuwa wamepumzika usiku huo msibani, ndipo mtu mmoja alipowaamsha ili wanywe chai.
Amesema alipoinuka, alimwamsha mama huyo lakini hakuitika.
“Licha ya kumtikisa mara kadhaa, hakuonesha dalili yoyote ya uhai, jambo lililotulazimu kuwaita ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa msibani hapo,” amesema Ruth.
Ameongeza kuwa, mmoja wa waombolezaji aliita gari kwa ajili ya kumkimbiza hospitalini mama huyo, lakini baadaye ilibainika kuwa alikuwa tayari amefariki dunia.
"Shangazi yangu nilitoka naye Kiboriloni kuja huku msibani na tulipofika, alisema hatarudi Kiboriloni tuungane na waombolezaji wengine, hivyo tulilala pale msibani kwa kuwa huyu aliyefiwa ni jirani yetu, hivyo hatukuondoka.
“Wakati tumekaa huyu shangazi yangu akasema mtu anazikwaje bila kichwa? Shangazi akaanza kama kulia hivi, akanyanyuka na kwenda kuangalia picha ya marehemu, nikamwambia tumwachie Mungu, basi tukakaa pale, tukalala, baadaye kuna mtu alikuja kutuamsha, shangazi naye akaamshwa, hakuamka na wala haongei, hivyo tukaanza kumpa huduma ya kwanza hakuamka wala kujigusa na tulivyomfikisha hospitali tayari alikuwa ashafariki," amesema.
Akizungumza binti wa marehemu, Laitenes Ngowi amesema kuwa wakati mama yake anaondoka nyumbani kwenda msibani alikuwa na afya njema na hakuwa na tatizo lolote.
"Baada ya muda nikasikia mtu anagonga nyumba, nikachungulia kwenye dirisha nikaona ni yule yule aliyeondoka naye, nikasema labda mama harudi amelala.
“Nilipomfungulia nikamwambia mama yuko wapi mbona umerudi mwenyewe, akanambia mama yako kazimia, akaniuliza mama anashida yoyote ya kudondoka? nikamwambia hapana mama hajawahi kudondoka na hana tatizo lolote la presha na sijawahi kuona hiyo hali hata siku moja.
"Niliondoka kwenda msibani na nilipofika kumgusa mama,akawa hahemi wala haongei na hafanyi chochote, basi wakati huo tayari alishatafutwa mtu wa gari kumpeleka hospitali, kushika miguu ya mama tayari ilishapoa nikawa najipa moyo, tulienda Hospitali ya Mawenzi moja kwa moja, tulipofika pale tukaambiwa wamejaza, hivyo tukaenda Hospitali ya St Joseph tulipofika mama akapimwa wakasema alishakufa muda mrefu sana," anasimulia mtoto huyo.