Mzazi mmoja, talaka mzigo kwa Serikali

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjiri la Kirutheri Tanzania (KKKT) Dk Fredrick Shoo.

Muktasari:

  • Mkutano wa kimataifa wa Afya ya Msingi umeelezwa kuhusu ongezeko la tatizo la afya ya akili kwa wajane, waliopewa talaka na ‘single mother’ (mlezi mmoja),  kwamba umekuwa mzigo kwa Serikali kwa muda mrefu. Pia, mmoja wa washiriki ametaka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwekwe jina la Mungu.

Dodoma. Mkutano wa kimataifa wa Afya ya Msingi umeelezwa kuhusu ongezeko la tatizo la afya ya akili kwa wajane, waliopewa talaka na ‘single mother’ (mlezi mmoja),  kwamba umekuwa mzigo kwa Serikali kwa muda mrefu.

Pia, washiriki wa mkutano unaozungumzia umuhimu wa Afya ya Msingi, wamezungumzia haja ya kuzitambua tiba asili kwa ngazi ya chini na mwingine ametaka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwekwe jina la Mungu kwa tangu mwanzo wa hadi mwisho hakuna jina Mungu.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Machi 26, 2024 kwenye mada iliyohusu namna dini zinavyojihusisha na Afya ya Msingi katika jamii.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk Zaituni Hamza ndiye ameibua hoja inayohusu ustawi wa jamii kwamba haijajadiliwa kwenye mkutano huo kwa  kuwa Serikali inabeba mzigo wa tatizo la afya ya akili kwa wajane, waliopewa talaka na ‘single mother.’

“Viongozi wa dini naona hapo mbele kuna Askofu Shoo ( Dk Fredrick aliyewahi kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Sheikh Othman (Zubeir, ambaye ni Katibu wa Vijana kutoka Baraza la Waislamu Tanzania – Bakwata), watueleze kuna tatizo gani kuhusu ongezeko la talaka hasa kwa vijana na tatizo la ‘single mother’?” amesema Dk Hamza.

Pia, amesema kuna tatizo la ‘single mother’ kuongezeka kwa kasi na hiyo inatokana na mtu kujitangaza na kutaka wengine wawe kama yeye, na wengie wao ndio wanafika kwenye  vituo vyao vya ustawi wa jamii kutafuta huduma.

“Kama wewe umeshindwa, usilazimishe na wengine wawe kama wewe, mimi ni ‘single mother’ au mimi nisizae mtoto, haikubaliki,” amesema kwa msisitizo Dk Hamza.

Akijibu swali hilo, Askofu Shoo amesema tatizo ni maadili na lishe inayotakiwa. “Hili si suala la viongozi wa dini pekee ni letu sote. Familia imara inajengwa na mila na desturi, tukiwa na familia imara tutakuwa na jamii imara.

“Misingi ya kuporomoka kimaadili ni kuporomoka kiroho. Lakini, ulaji sahihi siku hizi kuna tatizo la kupungua nguvu za kiume ndoa zitaacha kuporomoka. Na hii inasababishwa na ulaji usio sahihi, chipsi mayai, mtu unakula chipsi mayai,” alisema Askofu Shoo.

Kwa upande wake Kaimu mkuu wa Jumuiya ya Lutheran kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Shirikisho la Dunia la Lutheran, Loe Rose Mbise amesema tatizo la talaka kuwa nyingi linatokana na wanandoa kukosa malezi ya asili ambayo walikuwa wakifuatiliwa maisha yao kwa muda wote.

“Zamani mtoto anazaliwa hadi anakuwa alifuatiliwa maisha yake, baada ya kuja elimu ya darasani tatizo likaanza hapo, siku hizi familia haziko pamoja, mtoto anaishi mabali na wazazi wake. Baba anaishi mji mwingine na mtoto anaishi mji mwingine,” amesema Mbise.

Pia, amesema zamani watoto wanapooana walifuatiliwa maisha yao na pailipokuwa na tatizo walielekezwa tofauti na sasa, ameshauri kuanzishwe maeneo ya kutoa ushauri.

Kuhusu viongozi wa dini kushughulikia masuala ya ndoa amesema, viongozi wa dini wengi ni wanaume nap engine inakuwa shida kwa wanawake  kwenda kujieleza kwao.

Sheikh Othman amesema tatizo ni maadili na kwamba Sheikh Mkuu, Mufti wa Tanzania, Sheikh Dk Abubakar Zubeir kutokana na malalamiko mengi ya talaka yaliyopo kwenye ofisi ya Mufti amelazimika kuunda timu ya kufanya uchunguzi wa tatizo hilo.

“Ofisini kwa Mufti kuna malalamiko mengi ya talaka ambayo yamemshitua, hata Waziri Gwajima (Dk Dorothy Gwajima ambaye ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum) alikuja ofisini kwa Mufti kuuliza chanzo cha tatizo la talaka. Uchunguzi umekalika na ripoti itatoka hivi karibuni,” amesema Sheikh Othman.

Katiba na jina la Mungu

Hoja ya Katiba iwe na jina la Mungu imetolewa na Dk Godfrey Mtey amesema kuna haja ya kuweka ndani ya Katiba jina la Mungu kwa kuwa tangu ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho hakuna jina la Mungu ndani ya Katiba.

“Kuna umuhimu wa kumtanguliza Mungu, Katiba yetu iwe na jina la Mungu. Mfano, fedha ya dola ya Marekani ina neno; ‘In God we Trust’ tunamwamini Mungu,” amesema.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii amesema Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Nyerere aliliona hilo na ndio maana kwenye wimbo wa Taifa kuna jina la Mungu klluanzia mwanzo hadi mwisho.

“Kwenye Katiba ya Warioba (Jaji Joseph Warioba) walitaka kuweka wimbo wa Taifa ndani ya Katiba, ikaleta shida kwa kuwa Zanzibar nao wana wimbo wao wa Taifa, lakini ingewekwa yote tu,”: amesema Dk Mtey ambaye ni mganga mkuu wa mkoa mstaafu.

Kwa upande wake Dk Valentino Bangi ambaye kwa sasa ni mhadhiri wa Chuo  Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tanzania, amesema kuna umuhimu katika Afya ya Msingi kuwaweka watalaamu wa tiba asili.

“Zamani hawa ndio walikuwa wanatoa tiba, kama ni nzuri au mbaya lakini ndio  waliokuwepo, sasa kuna haja ya kwenda nao,” amesema.

Akijibu hoja hiyo, Dk Paul Chaote ambaye ni Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), amesema wataalamu wa tiba asili wapo ngazi ya Taifa na mikoa na kwamba huko chini hawapo kutokana na uhaba wa wataalamu.

“Wataalamu tulionao wamesoma China na huko wamesoma miti shamba ya China na si Tanzania, hivyo tuna changamoto ya kusomesha wataalamu wetu nchini,” amesema.