Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Naibu katibu mkuu apiga marufuku kutorosha mifugo nje ya nchi

Naibu Katibu mkuu Mifugo, Dk Daniel Mushi akizungumza na wafugaji katika mnada wa Meserani mkoani Arusha alipotembelea mnada huo.

Muktasari:

  • Naibu Katibu Mkuu Mifugo ameutaka uongozi wa Wilaya ya Longido kudhibiti utoroshaji wa mifugo nje ya nchi.

Arusha. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo, Dokta Daniel Mushi ameutaka uongozi wa Wilaya ya Longido kujipanga  na kuweka  doria  za kutosha mipakani ili kuzuia  utoroshaji wa mifugo ambayo inapelekwa  nchi jirani ya Kenya  na kupelekea  kuwepo kwa upungufu  wa mifugo nchini.

Ameyasema hayo leo Agosti 30 jijini Arusha akiwa katika ziara yake  ambapo ametembelea  mnada  wa mifugo katika eneo la Meserani pamoja na kiwanda cha kuchakata nyama cha Elia food Overseas  kilichopo  Wilaya ya Longido  mkoani Arusha.

Dk  Mushi  amesema kumekuwepo na uhaba mkubwa wa mifugo hapa nchini hivi sasa changamoto inayopelekea  kushuka  kwa soko la mifugo kutokana na utoroshaji  wa mifugo hiyo kwenda nje ya nchi jambo ambalo linaikosesha serikali hasara kwani haipati mapato yoyote.


"Jamani katika hili nawaagiza viongozi wote wa Wilaya ya Longido mkae  pamoja na kuunda timu maalumu ya kufanya doria katika maeneo ya mipakani ili kudhibiti  utoroshaji  huo ambao unafanywa na wafugaji kwa lengo la kutafuta soko nje ya nchi kwa njia  zisizo  halali jambo ambalo linaikosesha serikali mapato yake na kuendelea kupungua  kwa Mifugo hapa nchini," amesema Dk Mushi. 

Amewataka viongozi hao pia kukaa na Wazee wa kimila (Malwaigwanan) ili kuweza kuwaelimisha watoe elimu kwa jamii zao za wafugaji kuhusu madhara  ya utoroshaji kwani mifugo, inapotoroshwa serikali ndiyo inapata  hasara kubwa.

"Moja ya changamoto iliyoelezwa kuchangia kuwepo kwa utoroshaji ni ukosefu  wa maji kwa ajili ya kulishia  malisho  hayo, sisi kama Serikali tutaangalia namna ya kujenga mabwawa  ya kutosha na naombeni halmashauri pamoja na wawekezaji waangalie  namna ya kujenga mabwawa ya kutosha ili mifugo isitoroke nchi jirani," amesema.

Aidha amewataka wawekezaji  kuboresha bei  zao wanazonunulia  mifugo hapa nchini ikilinganishwa na nchi jirani kitendo kinachopelekea  mifugo mingi kukimbilia  huko, hivyo kuwataka kuboresha bei zao ili wafugaji wauze mifugo yao  hapa nchini na kuondokana na uhaba huo.

Wakurugenzi wa Kiwanda cha Eliya food Overseas Ltd, Shabbir Virjee na Irfhan Virjee wamesema kuwa, hivi sasa wamepunguza uzalishaji kiwandani  kutokana na upungufu wa Mifugo ambayo nyingi inapelekwa nchi jirani na hivyo kupelekea  wao kukosa soko hilo na hivyo kuishia kupata hasara kubwa.

Irfhan amesema kipindi cha nyuma walikuwa wanachakata mbuzi na kondoo elfu nne  kwa siku ambayo ni sawa na tani hamsini kwa siku ambapo  baada ya kupata  changamoto  ya ukosefu wa  mifugo kuanzia  mwezi sita  na kufanya uzalishaji kushuka na kufikia mbuzi na kondoo mia tano kwa siku kutokana na mifugo hiyo kuuzwa nje ya nchi.

Baadhi ya wafugaji wakizungumzia changamoto hiyo, waliomba Serikali kuwaboreshea  mazingira  mazuri kwa wawekezaji  hapa nchini ili waweze kuuza bei nzuri kama ambavyo nchi jirani  ya Kenya inafanya  kununua  mifugo  kilo  Sh14,000 tofauti na hapa nchini ambapo wananunua kwa kilo Sh9,300.