Najiuliza mke wangu amenipa nini? Nisipomuona nachanganyikiwa

Muktasari:
- Nimeoa huu mwaka wa nne, lakini nashindwa kumzoea mke wangu, kiasi kwamba nahisi ni kiboko yangu. Akiwa likizo ninakuwa kama paka wa jikoni, muda wote namzunguka kiasi cha kubadili muda wa kuchukua likizo mara kwa mara ili niwe naye.
Nimeoa huu mwaka wa nne, lakini nashindwa kumzoea mke wangu, kiasi kwamba nahisi ni kiboko yangu. Akiwa likizo ninakuwa kama paka wa jikoni, muda wote namzunguka kiasi cha kubadili muda wa kuchukua likizo mara kwa mara ili niwe naye.
Nikiwa kazini ninapata shida sana kwa sababu naona muda hauishi ili nikamchukue kazini kwake turudi nyumbani. Napata wivu wa ajabu hata nikimuona anazungumza na kaka zake.
Anti naomba kujua hivi kweli duniani kuna limbwata? Nahisi nimewekewa, haya si mapenzi ni wazimu.
Kwanza kabisa achana na mawazo ya limbwata sijui kurogwa, inavyoonekana umekolea mwenyewe kwenye penzi la maana unalopewa na huyo mwanamke. Aliyewekewa limbwata kama kweli lipo huwa hajijui, ni sawa na mwenye matatizo ya akili, siku akijijua ujue amepona. Unachotakiwa kufanya ni kupunguza kwanza wivu kwa sababu utakuwa unamdhalilisha mkeo, kama unamuonea hata akiwa na ndugu zake ni hatari utakapomkuta na jamaa yake usiyemjua, unaweza kuanzisha ugomvi.
Pili, kumpenda mkeo siyo dhambi wala uchawi, huyo ndiyo sehemu ya maisha yako na ukiachilia mbali familia yako unapaswa umpende kwa vyovyote iwavyo.
Kinachokutokea ni uhalisia wa mapenzi na ndiyo hasa maana ya kuwapo kwa hilo neno kupenda. Hakuna raha kama kupendana, huoni mnakuwa pamoja muda mwingi, ukimuona mtu anapenda kuwa mwenyewe ujue ana mambo mengine anafanya mbali ya yale ya familia.
Ila angalizo zingatia kazi kwa sababu ukiacha kazi utaona ilivyo ngumu kuipata.
Nimetoka naye siku moja sioni siku zangu
Anti nimefanya mapenzi na mwanamume siku moja, lakini sioni siku zangu na sina mpango wowote naye. Nifanyeje?
Tuliza akili yako, unadhani mimba inaingia siku ngapi. Pia katika karne hii unatembea na mwanamume bila kinga tena na mwanamume usiyekuwa na mpango naye? Sidhani kama unafikiri sawa sawa. Sina cha kukushauri kuhusu hiyo mimba ila nakukumbusha kutoa ni kosa na ukifanya hivyo utachukuliwa hatua za kisheria.
Wanawake wa aina yako ndio baadaye wanatangaza wananyanyaswa kumbe wanajinyanyasa wenyewe, mtu huna mpango naye unampa mwili wako aufanye anavyotaka tena bila kinga, siku nyingine usiniulize swali kama hili, maana linaudhi na halionyeshi ukomavu. Elimu kuhusu kujithamini inatolewa kila siku kupitia redio, mitandao ya kijamii, runinga na magazeti, kama haijakufikia mpaka sasa unahitaji maombi ya wiki saba.