Nani mbaya wa Paula?

Saturday February 20 2021
nani mbayapic5
By Kelvin Kagambo

Kinachotamba kwenye mitandao ya kijamii tangu Jumapili ya Februari 14 ni mkasa unaohusu video za msanii wa muziki kutoka lebo ya Wasafi, Rayvanny na binti maarufu kwa jina la Paula ambaye ni mtoto wa mcheza filamu nchini, Kajala Masanja na prodyuza wa muziki P Funk Majani.

Kama huelewi kinachoendelea ni kwamba, kuna video zilisambaa mtandaoni zikimuonyesha Rayvanny na Paula wakipigana mabusu kimahaba. Kusambaa kwa video hizo kunamuibua Kajala, na kumshushia tuhuma mwanamitindo Hamisa Mobetto kuwa ndiye aliyempeleka binti yake kwa Rayvanny, wakamnywesha pombe na kumrekodi hizo video.

Hata hivyo tuhuma hizo zilikanushwa na Hamisa kupitia Instagram yake na zaidi Hamisa Februari 16, alimtumia barua Kajala kupitia mwanasheria wake Eliya Rioba ya kutaka akanushe tuhuma hizo alizoziita za uwongo.

nani mbya paula piccc

Swali la msingi ni je, nani mbaya wa Paula, kati ya Rayvanny, Hamisa Mobetto na Kajala Masanja?

Maana kila upande unausukumia mwingine, huku watu wa mitandaoni wakishusha lawama.

Advertisement

Kajala

Mama mzazi wa binti huyo, mwigizaji Kajala Masanja anatuhumiwa zaidi kwenye sekeseke hili kuliko mtu yeyote yule. Wengi wanaomwangushia jumba bovu wanasema yeye ndiye sababu ya kila kilichotokea kutokana na malezi aliyokuwa akimlea binti yake huyo.

nani mbayapicccc3

Wengine wameandika; “Alikuwa akimlea binti yake kihuni,” huku wakitaja vitu kama vile video zilizowahi kusambaa mtandaoni zikimuonyesha akishindana na binti yake huyo kukatika viuno.

Tuhuma hizo pia zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na mzazi mwenzake, yaani prodyuza P Funk kumtuhumu Kajala kuwa ndiye anayemharibu binti yao, kutokana na aina ya malezi anayomlea, ikiwamo kumuanika mitandaoni.

Hamisa Mobetto

Ubaya wa Mobetto kwa Paula unatokana na alichokisema mama wa binti huyo kuwa yeye ndiye aliyemkutanisha na Rayvanny, kisha wakamlewesha pombe na wakamrekodi video hizo za ngono.

nani mbayapic3

Anashambuliwa na wachache akiambiwa amefanya jambo baya na yeye ana mtoto wa kike huenda kuna siku historia hiyo chafu ikajirudia kwa mwanaye.

Rayvanny

Waliomshambulia Rayvanny wanasema ubaya wake unatokana na swali la kwa nini alikuwa na mahusiano ya namna ile na mwanafunzi licha ya kwamba amevuka miaka 18.

Kama hiyo haitoshi, kwa nini aliposti video ile ya mahaba kwenye mitandao ya kijamii, akilaumiwa kuharibu maisha ya binti huyo ambaye inadaiwa alitakiwa kujiunga kidato cha tano Juni mwaka huu.

nani mbayapic5

Watu wengi waliomshutumu Rayvanny kwa uharibifu wakiwemo mastaa kama vile Harmonize, wametaka sheria ifuate mkondo wake kwa Rayvanny ili iwe funzo kwa wavulana wengine wenye tabia ya aina yake.

Paula

Ukiachana na idadi kubwa ya watu kumshambulia zaidi mama yake mtu wa pili kushambuliwa zaidi ni Paula mwenyewe.

Wengi wanamsimanga kwa kumuita majina kama vile ‘mapepe’ na kadhalika, huku wakidai tabia zake hazifanani na mwanafunzi na ndizo zilizomponza.

Wamelinganisha tabia zake na baadhi ya watoto wengine mastaa kama mtoto wa mwigizaji Monalisa anayeitwa Sonia na mwigizaji Khanifa Saidi, maarufu Jennifer Kanumba.

nani mbaya paupa pic

Mwanasaikolojia anasemaje

Akizungumza na Mwananchi, mwalimu wa saikolojia, Modesta Kimonga anasema kuna mambo matatu yaliyosababisha binti huyo afikie hatua hiyo, yakiwamo mazingira aliyokulia, makundi pamoja na uhusiano uliopo kati ya mzazi na mtoto.

Anasema kusambaa kwa video zile si kitu kigeni machoni mwa watu na hufanywa mara nyingi na wasanii. “Paula amekulia mikononi mwa wasanii, kwa hiyo kile kilichotokea kinaweza kuwa ni matokeo ya alivyoviona kwenye mazingira aliyokulia.

“Sote tunafahamu jinsi tabia za wasanii wengi zilivyo, kujirekodi video za mahaba kama zile si vitu vya ajabu. Kama mtoto anakua akiwa amezungukwa na watu wa aina hiyo haishangazi sana akifanya hivyo pia,” anasema Modesta.

Anasema makundi pia ni sababu ya binti huyo kuharibika, kwa mfano, urafiki wa binti huyo na Hamisa Mobetto, ambao wanatofautiana umri ni dalili mbaya.“Hamisa ni mtu mzima sana kuwa na urafiki wa karibu na Paula. Kwa hiyo kama makundi anayojihusisha nayo ni ya watu kama kina Hamisa na wasanii wengine ambao kwao ni kawaida kujirekodi video za kimapenzi, usitegemee huyu mtoto kufanya tofauti na hivyo,” anasema Modesta.

Anasema jamii, wazazi ndiyo wabaya wa binti huyo kwa kuishi naye kama mtu mzima ilihali wanajua ni mdogo.

“Hapa baba na mama wa Paula wanabeba lawama hii kwa kushindwa kutimiza wajibu wao kama wazazi na kumkabidhi binti yao katika mikono ya dunia alelewe. “Najua wanalijua hili, mtoto halelewi mitandaoni, hata kama anapendwa vipi, kama wao kuna wakati inawanyima usingizi vipi wamkabidhi binti yao”anasema na kuhoji.
Advertisement