Ndingo ataja sifa za kiongozi anayefaa Mbarali
Muktasari:
- Wakati wananchi wa Mbarali wakitarajia kufanya uchaguzi mdogo Septemba 19, 2023 mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, Bahati Ndingo ametaja sifa anazotakiwa kuwa nazo kiongozi ikiwemo kujenga hoja na kushaiwishi Serikali kutatua changamoto za jimbo hilo.
Mbarali. Mgombea ubunge wa Mbarali kwa tiketi ya CCM, Bahati Ndingo amesema utatuzi wa kero za wakazi wa jimbo la Mbarali unahitaji kiongozi asiye na misuli ya kupambana, bali mwenye kujenga hoja nzuri, mchapakazi na mtu huyo ni yeye.
Amesema changamoto za maji, ardhi na umeme na miundombinu ya barabara zinamuhitaji anayejua namna ya kuishawishi Serikali ili kuzitatua hivyo amewaomba wananchi wampigie kura katika uchaguzi utakaofanyika Septemba 19, 2023.
Ndingo ameeleza hayo leo Jumamosi Septemba 16, 2023 wakati akiomba kura za kuwa mbunge wa Mbarali kwa wananchi wa Luwango- Matemela, Isunura, Utyego, Madibira katika mwendelezo wa mikutano yake ya hadhara ya kampeni ya kuwania kiti hicho.
Uchaguzi huo unafanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega aliyefariki dunia Julai Mosi mwaka huu, shambani kwake wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji hivyo, Ndingo amesema ana uwezo wa kulitumikia jimbo hilo ikiwemo kujieleza, kujenga hoja bungeni ili changamoto za wananchi wa Mbarali zipatiwe ufumbuzi.
"Nitumeni nina uwezo, hizi changamoto za barabara najua kuzijengea hoja na kupatiwa ufumbuzi, najua wapi pakupita.Nitakwenda kuhimiza watendaji wa Serikali waje kutimiza majukumu yao ya kutatua changamoto hizi.
"Nilijitithamini na kufanya uamuzi wa kugombea jimbo la Mbarali, lakini nilichogundua changamoto za jimbo letu hazihitaji misuli bali ujengaji thabiti wa hoja za kuzieleza na kuchanganua matatizo haya ili kupata mwarobaini," amesema Ndingo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu.
Katika ziara hiyo, Ndingo aliambatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Ndele Mwaselela aliyewataka wananchi wa Mbeya kutokuwa na wasiwasi na mgombea wao akisema kila kitu kitakuwa sawa katika kuleta maendeleo wilayani humo.
Kuhusu changamoto za barabara, Mwaselelaa amesema endapo Ndingo akifanikiwa kuibuka kidedea atashirikiana naye ili ndani ya siku 60 barabara mbalimbali zikiwemo za vijijini zichongwe ili kupitika kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa.
"Suala la uboreshaji wa barabara litafanyika ndani ya siku 60 nitazungumza na Serikali ya mkoa kuandaa utararibu bora wa kuboresha miundombinu hii, tumesikia kilio chenu wananchi wa Mbarali.
Mwaselela ambaye ni mdau wa masuala ya elimu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa gari la kuchimba visima, mkoani Mbeya hivi sasa lipo Chunya likitoka huko linakwenda Mbarali kuchimba visima ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo.
"Wakati tukisubiri mradi wa kudumu wa upatikanaji wa maji ya uhakika, tutachimba visima, nyie mpigieni kura Ndingo kwa wingi. Hivi mimi MNEC naweza kuwadanganya kwamba hatutashughulikia kero zenu, ukizingatia mwakani ni uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.
"Niwahakikishie tutazichukua changamoto zenu zote ili kuzipatia ufumbuzi," amesema.
Mwaselela amesema atazungumza na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhusu upatikanaji wa maji katika maeneo mengine ili kujua mipango ya Serikali la kutatua changamoto hiyo katika maeneo mbalimbali wilayani.