Ni fainali Siha na Kinondoni
Muktasari:
Mbali ya majimbo hayo kuchagua wabunge, pia wananchi wa kata tisa watachagua madiwani baada ya nafasi hizo kuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.
Dar/Moshi. Wananchi katika majimbo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro leo wataamua nani awe mbunge wao kwa kipindi cha miaka mitatu iliyobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu 2020.
Mbali ya majimbo hayo kuchagua wabunge, pia wananchi wa kata tisa watachagua madiwani baada ya nafasi hizo kuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.
Kata hizo ni Isamilo ya Wilaya ya Nyamagana, Manzase (Chamwino), Madanga (Pwani), Mitunduruni (Singida), Kanyelele (Misungwi), Buhangaza (Muleba), Donyomurwak, Garagua na Kashashi za Siha.
Jumla ya vyama 12 vinashiriki uchaguzi huo ambavyo ni CCM, Chadema, TLP, Sau, Demokrasia Makini, UMD, DP, CUF, NRA, CCK, AFP na Ada.
Uchaguzi wa ubunge katika majimbo hayo mawili unafanyika baada ya waliokuwa wabunge wake, Maulid Mtulia (CUF – Kinondoni) na Dk Godwin Mollel wa (Chadema – Siha), kuvihama vyama vyao na kutimkia CCM hivyo kupoteza nyadhifa zao.
Kwa zaidi ya wiki tatu sasa, vyama hivyo vimekuwa vikiminyana katika kampeni zilizokuwa zikifanyika katika maeneo mbalimbali ya majimbo hayo pamoja na kata hizo huku viongozi wake waandamizi wakiwanadi wagombea wao ili kujihakikishia ushindi wa kishindo.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema uchaguzi huo mdogo wa ubunge pamoja na kata tisa una maana kubwa kwa kuwa utakuwa kipimo cha demokrasia.
Wanasema utakuwa kipimo cha namna wakazi wa majimbo hayo wanavyofikiri na kufikia uamuzi lakini pia matokeo ya uchaguzi kwenye majimbo hayo yatakuwa ni kielelezo cha jinsi walivyowapima wagombea na ajenda zao.
Tume yaonya wasimamizi
Ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa wote, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewataka wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kutumia weledi wao katika kusimamia uchaguzi ili kuiwakilisha vyema.
Imesema endapo wasimamizi hao wataboronga uchaguzi huo, lawama zote zitaishukia NEC.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura katika Jimbo la Siha, mjumbe wa NEC, Jaji mstaafu Mary Longway alisema wasimamizi hao ndiyo wenye dhamana ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanikiwa.
“Nyie ndiyo tume mkiboronga, imeboronga Tume. Mtakayosababisha nyie lawama inakwenda kwa tume; naomba sana mzingatie weledi. Uchaguzi wa mwaka 2015 siyo kama huu. Huu ni uchaguzi mdogo, una mazingira ya kubadilika kutegemea mambo mbalimbali na mawazo ya watu, kwa hiyo zingatia weledi katika kufanya kazi yako. Kama msimamizi wa kituo, hakikisha sikio lako linasikiliza kinachosemwa na kinachotamkwa pale,” alisema.
Aliwataka wasimamizi hao kuhakikisha wanawapa maelekezo sahihi watu wanaowasaidia wapigakura wenye mahitaji maalumu kama wasiojua kusoma na kuandika na wenye ulemavu.
Awali, mkurugenzi wa habari na elimu ya mpiga kura wa NEC, Giveness Aswile aliwataka wasimamizi wa vituo kuendesha uchaguzi kwa haki na amani na kueleza juu ya matumizi sahihi ya fomu za uchaguzi ikiwamo namba 18 inayomruhusu wakala wa chama cha siasa kupiga kura nje ya kituo alichojiandikisha.
Kuhusu matumizi ya vitambulisho mbadala, mkurugenzi huyo alisema msingi wa kwanza ni, “lazima uwe umeandikishwa katika daftari la wapiga kura kwa hiyo ile hoja kwamba nitaipata wapi namba yake, hutajaza namba ya pasipoti, ile inamsaidia tu. Kwamba si unamuona katika daftari na kwenye orodha mfano Ally Salimu Juma yupo lakini bahati mbaya kitambulisho alipoteza kwa hiyo msingi wa kwanza ni lazima awepo katika daftari.
“Siyo daftari la Tume ni daftari la kituo. Inawezekana yupo pahali pengine lakini siyo pale kwa hiyo kwanza ujiridhishe yupo. Je, pasipoti aliyoleta au kitambulisho cha Nida majina yanawiana? Kwa hiyo wewe unamjazia namba ile iliyopo katika daftari kile kitambulisho alichokuja nacho kimemsaidia kujitambulisha tu.”
Polisi Moshi/ Dar wajipanga
Sambamba na angalizo hilo la NEC kwa wasimamizi wa uchaguzi huo, Jeshi la Polisi limesema limejipanga kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu.
Katika Jimbo la Siha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema jeshi hilo limejiandaa na kuwatoa hofu wananchi watakaoshiriki katika uchaguzi huo.
Kamanda Issah alisema wamejipanga kuzunguka maeneo mbalimbali hivyo wananchi wasiogope kwa kuwa lengo lao ni kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika na si vinginevyo.
“Msitishike, Jeshi la Polisi liko kwa ajili yenu na tutahakikisha usalama upo wa kutosha kabla na baada ya kupiga kura, wakati wa kuhesabu na wa kutangaza matokeo kwa kuwa ni hatua ambazo zote zinahitaji ulinzi wa uhakika,” alisema na kuongeza:
“Tunawasihi wananchi pindi mtakapomaliza kupiga kura zenu nendeni nyumbani msubiri matokeo. Vitendo vya kuanzisha vurugu vitawasababishia matatizo.”
Kwa upande wa Kinondoni, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema wamepata taarifa za kiintelijensia kuwa kuna kundi la watu wa chama fulani wamepanga kufanya vurugu na kuonya kuwa jeshi hilo litawashughulikia kwa mujibu wa sheria watakaojaribu kuharibu uchaguzi huo.
Alisema askari watakuwepo wa kutosha katika vituo vyote vya uchaguzi na ofisi za serikali za mitaa katika jimbo hilo na wataimarisha doria kwa kutumia magari, mbwa na farasi.
“Matokeo ya uchaguzi yanatolewa na vyombo vya habari, hivyo wananchi wanatakiwa kurudi majumbani mwao ili kusikiliza matokeo kupitia vyombo mbalimbali vya habari,” alisema Mambosasa.
Alivitaka vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kujiepusha na mikusanyiko kwenye vituo vya uchaguzi kwa sababu hairuhusiwi na jeshi lake limejipanga kuwadhibiti watakaokiuka amri hiyo.
Waliojiandikisha Siha ni 55,000
Akizungumzia wapigakura, msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Siha, Valerian Juwal alisema wananchi 55,313 wanatarajiwa kushiriki. Alisema vituo vya kupigia kura ni 160 na kwamba maandalizi yamekamilika kwa ajili ya uchaguzi huo wa mbunge na madiwani wa kata tatu za Donyomurwak, Kashashi na Gararagua.
Polisi watumia mabomu kutawanya maandamano ya Chadema
Polisi jana iliwatawanya kwa mabomu wanachama wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliokuwa wakiandamana jana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aaron Kagurumjuli.
Akizungumza jana kabla ya kuhitimisha kampeni za chama hicho zilizofanyika katika viwanja vya Buibui, Kinondoni, Mbowe alisema mpaka jana jioni mawakala wa chama hicho walikuwa hawajapewa barua za utambulisho na msimamizi wa uchaguzi.
“Jana (juzi) nilizungumza na Mkurugenzi wa Uchaguzi (Kailima Ramadhani) nikamweleza kwamba kuna tatizo mawakala wetu hawajapewa barua za utambulisho, akaahidi tungezipata leo asubuhi lakini mpaka sasa hivi saa 12 jioni hatujapata barua hizo,” alisema,
“Kutokana na hali hiyo hivi sasa tukitoka hapa twende kwa msimamizi wa uchaguzi kuchukua barua za utambulisho wa mawakala.”
Wanachama hao walianza kuandamana saa 12:05 jioni baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa kampeni kuelekea ofisi hizo zilizopo Magomeni.
Wakati wakielekea eneo hilo wakiwa wanapita Barabara ya Kawawa, Polisi walianza kuwazingira na walipofika eneo la Studio, magari ya polisi yaliongezeka na kufika matano.
Magari hayo yaliwapita wanachama hao na kwenda kuwasubiri eneo la Mkwajuni na walipofika walianza kufyatua mabomu na kutoa amri ya kusitishwa kwa maandamano hayo ambayo pia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji alikuwapo. Pamoja na zuio hilo, wanachama hao waliendelea kutembelea kuelekea Magomeni huku wakiimba na baadhi yao walikamatwa huku viongozi kadhaa wakiingia katika magari yao. Waandishi wa habari na wananchi wengine walilazimika kukimbilia katika nyumba za jirani na kwenye msikiti.
Mmoja wa wanachama hao, Paulina John alisema wamepoteza vitu vya thamani, zikiwamo fedha.
“Polisi wametuonea sana wangeacha tupewe viapo vyetu kama mawakala. Wametupiga mabomu tumeumia wengine tumepoteza simu na pesa,” alisema.
Juzi, Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho walikwenda makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kudai viapo vya mawakala wa chama hicho katika uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kinondoni.
Mawakala hao 613 waliapishwa bila kupewa viapo vyao jambo lililozua mvutano na msimamizi huyo wa uchaguzi huku wakielezwa kuwa wangepewa kabla ya Jumatano iliyopita.
Hata hivyo jana Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari alijibu hoja za Chadema kuhusu mawakala, kusisitiza kuwa taarifa alizonazo ni kwamba mawakala hao wameanza kupewa viapo vyao.
Imeandikwa na Tausi Mbowe na Peter Elias (Dar), Janeth Joseph na Florah Temba (Moshi)