No kushikwa. No mshiko

Muktasari:

  • Makengeza, Waswahili husema siku njema huonekana asubuhi. Sasa sijui siku mbaya pia? Au siku ya ugomvi na mikinzano huonekana alfajiri?

Makengeza, Waswahili husema siku njema huonekana asubuhi. Sasa sijui siku mbaya pia? Au siku ya ugomvi na mikinzano huonekana alfajiri?

Juzi nilikuwa nimejidamka mapema kwenda kununua mahitaji ya nyumbani kabla ya kwenda kazini. Kwa kuwa nilikuwa na haraka, nilifurahi kumkuta kijana ametandaza bidhaa zake chini karibu na sehemu ya kuingia sokoni.

Japo kulikuwa na vumbi kibao, si tungeziosha tu kabla ya kula. Lakini nilipotaka kuanza kununua, nilisikia sauti ya mwanamke nyuma yangu.

“Lakini wewe shemeji, mbona unataka kutuua hivyo?”

Nikashtuka na kugeuka na kumkuta jirani yetu. Nilijua kweli ana kibanda chake sokoni lakini nilikuwa nimesahau.

“Kwa nini nikuue shemeji?”

“Si unanunua vitu kwa huyu ambaye hana leseni, halipi ushuru wa soko, anaishi kwa kitambulisho ambacho kilienda zake na mwendazake. Tangu hawa waruhusiwe kupanga bidhaa popote, biashara yetu imedorora.”

Yule Machinga alikuja juu.

“Kwani na mimi sina haki ya kuishi? Mmechukua vibanda na vizimba vyote humu ndani, sasa tufanye nini?”

“Nakubali una haki ya kuishi lakini si kwa kuwaua watu wengine. Humu ndani tunalipa Sh300 kwa siku kwa vizimba vyetu sembuse kodi na tozo zote nyingine. Nyinyi mnakaa hapa bila kulipa ushuru wa aina yoyote lakini bado mtatumia na kuchafua vyoo vyetu, mtatumia na kuongeza dampo yetu lakini hamtoi hata senti tano. Kisha mnaua biashara zetu sisi tuliohangaika na kugharamika kujisajili.”

Machinga hakuwa tayari kusikiliza.

“Narudia. Sina haki ya kuishi? Sina haki ya kujikimu na mimi? Ama kweli Mwendazake kaenda na zetu pia.”

“Unayo haki lakini kwa kufuata taratibu.”

“Kama taratibu zinaniua inabidi nipambane nazo. Kuna vizimba humu ndani? Nitapata kizimba kweli bila kutoa chochote au lolote? Iwapo hakuna sehemu ya kupenya inabidi upenye kwa nguvu.

“Sasa watoto wangu hawana haki ya kuishi pia? Nipo hapa napambana na uonevu wote kila siku, matusi na kejeli za wewe na kaka zao kwa sababu ya wanangu. Niwalipia mahitaji yao yote ya shule na vijisenti ninavyopata hapa sokoni. Sasa unaninyima riziki.

“Shauri yako. Kila mtu apambane na hali yake. Nitakaa hapa na kuuza nyanya zangu maana hata mama yangu hutegemea hii biashara yangu. Ni mgonjwa sana na gharama za dawa zake hazisemeki. Wewe ni nani kunizuia?”

Basi Mmachinga akampa kisogo na kuendelea kupanga nyanya zake. Jirani yangu kidogo azipige teke maana hasira zilikuwa zimempanda.

“Nitazisambaratisha nyanya zako kama ambavyo unasambaratisha biashara yangu.”

Nikamshika asifanye kitu.

“Jamani, sisi maskini tukigombana wenyewe kwa wenyewe, itasaidia nini? Badala yake kwa nini tusigombane na ambao wanajaribu kutugombanisha. Wote mna haki ya kuishi, lakini siamini kwamba haki ya mtu inapaswa kuingilia haki ya mtu mwingine. Mtafute suluhu kwa pamoja. Tatizo ni kwamba bado tunaogopa kupaza sauti kwa waheshimiwa hivyo tunaishia kupambana mwishiwa kwa mwishiwa.”

Shemeji bado alikuwa amehemka na kuchemka, kwa hiyo nilimshika mkono na kumwongoza hadi kwenye kizimba chake ili angalau mimi ninunue pale.

Baadaye, kwa kuwa ilikuwa bado mapema nikaenda kwenye eneo la mama ntilie. Ndiyo mama ntilie, achana na wanaotulazimisha tusifurahie ubunifu wa lugha ya wananchi. Sasa baada ya kununua chai na vitumbua viwili, nikatulia. Kumbe ulikuwa umezuka ugomvi mwingine huko kwenye kibanda cha jirani. Nilimsikia binti akipaza sauti.

“Acha Bwana. Umenunua chai yangu. Hujaninunua mimi.”

Kule kijana mmoja alikuwa anacheka.

“No kushika no mshiko.”

Bahati nzuri wateja wengine waliingilia kati na yule kijana alilazimishwa kulipa kisha kuondoka. Kitendo hiki kikazua zungumzo. Mama Ntilie mmoja wa makamo akapaza sauti.

“Hawa mabinti wa siku hizi, ovyo sana. Yule si amejitakia tu. Anajipitisha akijitingishatingisha kisha anamwinamia ili mteja aone utajiri wote humu ndani. Hata mtakatifu atashawishika.”

Wazee wengine, wanawake kwa wanaume walikubaliana naye lakini mama mwingine akapaza sauti na yeye.

“Lakini wewe Mama Wawili acha unafiki. Si ni wewe ulimshauri mwenzio juzi atafute kabinti karembo kadogodogo kisha umvalishe nguo fupi zinazobana ili kuwavutia wateja? Na huyu Chaupele wako hapa? Hakutaka kabisa kuvaa hiyo sketi fupi lakini wewe ulimwambia nini? Vivyohivyo kama yule kijana. No kushikwa no mshiko. Unajua kwamba kushikwa kwake kunakuongezea kipato hivyo uko tayari kutomlipa kama hataki kuwa mshawishi. Sasa kweli unageuka na kumlaumu akishikwa? Au umekasirika kwa sababu yule binti amemshinda Chaupele wako? Tuache unafiki Mama Wawili.”

Zogo likawa zogo maana Mama Wawili kumbe ni kiongozi wa akina Mama Ntilie na mjumbe wa kamati ya soko. Akajaribu kutumia cheo chake kama silaha.

“Nitakufukuza. Nitakufukuza hapa. Unanikashifu namna hiyo. Nitahakikisha unasimamishwa miezi mitatu.”

Mwenzake akajibu.

“Thubutu. Mwone Chaupele. Hana hata raha.”

Mama Wawili akazidi kujifunga kibwebwe na kutishatisha lakini mwanamume mmoja ambaye alikuwa amekaa pale akinywa supu akasema.

“Mama Wawili, usikatae ukweli. Kwani hatujui? Tunajua si wewe tu bali ni mtindo hapa. Mabinti walio wengi hapa wanakuja ili wapate kujikimu lakini nyinyi akina mama wazee, badala ya kufunza na kuwalinda, mnawalazimisha kuingia hatarini wenyewe. Ogopa Mungu Mama Wawili.”

Akageuka na kupaza sauti.

“Na nyinyi nyote vivyohivyo. Tuwalinde na kuwalea mabinti zetu badala ya kuwaingiza hatarini kisha kuwalaumu na kuwahukumu wakipata matatizo.”

Mama Wawili alilazimika kushusha mihemko.

“Lakini kama wote wanafanya hivyo ili kuongeza biashara, na mimi nitafanyaje?”

Yule mzee alicheka.

“Jamani si mna umoja wenu. Badala ya kushindana kwa uovu, kwa nini msipitishe kanuni yenu kwamba ni marufuku kulazimisha mabinti wafanyakazi wenu kuwa na nguo na tabia za kuwashawishi wateja kuwashika. Na akiwepo binti mwenye tabia ya kufanya hivyo, aambiwe aondoke. Na mteja katili afukuzwe kabisa. Mkisimama imara kwenye maadili yenu, mtashinda na mtashangaa mtaongeza wateja. Unafikiri sisi wateja wengine tunafurahi kuona huo uonevu?”

Wote kimya. Nikamaliza vitumbua vyangu na kujiondokea. Kwa nini sisi waishiwa hatujui jinisi ya kuungana ili kulenga hasira zetu kwa wenyewe badala ya kuogopa na kuelekeza hasira kwa wengine.

Lakini nilipofika kazini nikakuta wenzangu nao wanataka kuungana kweli.

“Yaani hizi posho ni uonevu kabisa. Leo tunaambiwa kupitia upya mpango kazi wetu ili kuzingatia viwango vipya vya posho.”

“Kwani kuna ubaya gani. Ni agizo la serikali.”

“We Bwana ulizaliwa wapi. Ona hapa. Robo tatu ya safari zetu za kikazi zimefutwa ili kutunisha mfuko wa posho ya mabosi. Tutafanyaje kazi hivyo?”

Wakaanza kuimba.

Bosi mamilioni

Sisi kilioni

Bosi mamilioni

Sisi kilioni.

Tuliombwa wote kusaini barua ya kuomba mkutano na bosi ili tujadili hili suala. Dah! Nikakumbuka ushauri wangu kule sokoni. Umoja ni nguvu. Lakini mmmmmmh! Rahisi kushauri, kwa nini hatutendi?

Jamani swali hili nawatupia nyinyi. maana nimeshindwa kujibu Kwa nini hatutendi?