Ntibazonkiza ni balaa tu Yanga
Muktasari:
Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameendeleza kasi yao ya kusaka ubingwa msimu huu baada ya jana kuifumua Ihefu FC kwa mabao 3-0, mchezo uliofanika kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya
Mbeya. Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameendeleza kasi yao ya kusaka ubingwa msimu huu baada ya jana kuifumua Ihefu FC kwa mabao 3-0, mchezo uliofanika kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ushindi huo umenogeshwa zaidi na nyota mpya wa miamba hiyo ya Jangwani, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, ambaye katika mchezo wake wa pili ametoa pasi tatu za mabao hadi sasa.
Mchezo wa kwanza wa Saido ulikuwa dhidi ya Dodoma Jiji, ambao aliingia kipindi cha pili na kufunga bao la pili na kutoa pasi ya la tatu kwenye ushindi wa 3-1.
Katika mchezo wa jana, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Burundi alipiga chenga mabeki wawili na kumpa pasi safi Deus Kaseke, ambaye alitulia na kumfunga kiufundi kipa wa Ihefu, Deogratias Munish ‘Dida’.
Miamba hiyo ya Dar es Salaam ilikwenda mapumziko ikiwa na uongozi wa bao moja.
Vijana wa kocha Zuberi Katwila walikuwa na mchezo mzuri huku wakiwa na nyota wapya kama Simchimba, Juma Mahadhi na Dida akiwa langoni lakini makosa machache waliyoyafanya yaliwagharimu.
Yanga ilianza tena kwa kucheza kama kocha Cedric Kaze alivyokuwa akitaka kwa kuanza kwa pasi kutengeneza nafasi.
Saido tena, akipokea mpira mbele kidogo ya eneo la katikati aligeuka haraka na kupiga pasi nzuri kwa Yacouba Sogne aliyecheza kama mshambuliaji wa kati jana, ambaye aliuwahi na kuingia kumtafuta kipa wa Ihefu, Dida aliyepigwa chenga kabla ya mpira kuwekwa kimiani.
Bao hilo lilikuwa la tano kwa Yacouba msimu huu, kabla ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kufunga la tatu akizima mchezo.
Kaze amekuwa mwenye mafanikio zaidi kwa timu yake kucheza huku ikipata mabao mengi.
Katika michezo mingine ya jana, JKT Tanzania imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, wakati Mtibwa Suhar ikifumuliwa nyumbani kwa bao 1-0 na Dodoma Jiji mkoani Morogoro.