Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyabiyonza mabingwa Bashungwa Karagwe Cup 2024

Muktasari:

  • Mashindano ya Bashungwa Karagwe Cup 2024 yameendelea kuwa chachu ya michezo nchini ambapo bingwa wa msimu huu amejinyakulia Sh6 milioni.

Karagwe. Timu ya Nyabiyonza imetwaa ubingwa wa Bashungwa Karagwe Cup 2024 kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuifunga Ndama mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa  Uwanja wa Bashungwa uliopo Kayanga Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Mbunge wa Karagwe ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa yalizikutanisha timu 23 kutoka kila Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambapo yalihitimishwa jana Agosti 25, 2024.

Nyabiyonza wameibuka na kitita cha Sh6 milioni, medali za dhahabu, seti moja ya jezi pamoja na kombe huku mshindi wa pili akijipatia Sh4 milioni, medali ya shaba na seti moja ya jezi.

Mshindi wa tatu timu ya Kihanga wamejipatia Sh2.5 milioni, medali pamoja na seti moja ya jezi huku mshindi wa nne timu ya Nyakakika akijipatia Sh1.5 milioni.

Zawadi zingine katika mashindano ni kwa kipa bora aliyejipatia Sh 100,000, wafungaji bora watano kila mmoja Sh100,000. Kwa upande wa mchezaji bora wa mashindano (MVP), amejipatia kiatu mfano wa kombe na kiasi cha Sh100,000 wakati mchezaji aliyecheza mchezo wa kiungwana (Fair Play), akijinyakulia zawadi ya mpira.

Akizungumza wakati akihitimisha michuano hiyo ya Bashungwa amempongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya michezo hususani mpira wa miguu.

“Na mimi niliona kwa Dira nzuri na maono ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kukuza michezo nchini, nikaona hapa Karagwe tusibaki nyuma ndio maana tunaendelea kuboresha ligi yetu ya Bashungwa Karagwe Cup,” amesema Bashungwa.

Bashungwa ameahidi kuendelea kuboresha mashindano yajayo ili kuwa na chachu zaidi na kuleta mafanikio kwa kuwa lengo la mashindano hayo ni kuimarisha afya kwa vijana, kusaka vipaji na kuviendeleza kwa kuunda timu ya Halmashauri itakayoshiriki katika ligi mbalimbali ndani na nje ya Wilaya ya Karagwe.

Hata hivyo, Mbunge huyo amepokea ombi la kuanzishwa kwa mashindano madogo ndani ya mashindano ya Bashungwa Karagwe Cup kwa michezo ya wa Mpira wa Pete (Netball), mchezo wa ngumi (masumbwi), na mpira wa meza (table tennis).

Naye, Mratibu wa Ligi ya Bashungwa Karagwe Cup, Johnson Majara ameeleza kuwa mashindano hayo ni muendelezo wa mashindano yaliyoanza tangu mwaka 2017 ambapo kwa mwaka 2024 yalishirikisha timu kutoka kata 23 za Wilaya ya Karagwe zilizopangwa katika makundi sita na mpaka kufikia fainali.