Nzige walioingia Tanzania waangamizwa
Muktasari:
Serikali imesema nzige wa jangwani walioingia nchini Tanzania Februari 19 mwaka huu wakitokea nchi jirani ya Kenya wameangamizwa wote.
Moshi.Serikali imesema nzige wa jangwani walioingia nchini Tanzania Februari 19 mwaka huu wakitokea nchi jirani ya Kenya wameangamizwa wote.
Hayo yamesemwa leo Machi 9 ,2021 na Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda wakati alipoulizwa na Mwananchi kuhusu uendelevu uteketezaji wa nzige hao.
Nzige hao waliokuwa makundi kwa makundi walivamia maeneo mbalimbali hapa nchini zikiwemo Wilaya za Mwanga, Siha , Monduli, Longido ambao yalizua taharuki kwa wananchi wa maeneo hayo wakihofia kuleta madhara.
Hata hivyo, serikali imesema mpaka sasa nzige hao ambao walikuwa makundi kwa makundi hawajasababisha madhara yoyote kwa wananchi.
"Tatizo la nzige limeisha na tumewaangamiza nzige wote, tunachokifanya sasahivi ni kuangalia maeneo ambayo nzige hao walitua kama waliacha mayai ili tuyaangamize," amesema Profesa Mkenda.
Februari 19 mwaka huu , Serikali ilitangaza rasmi uwepo wa kundi la wadudu aina ya nzige zaidi ya milioni 50 walioingia nchini kupitia Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro na baadaye kuelekea Wilaya za Simanjiro, Siha,Longido na baadaye Wilaya ya Monduli ambapo nzige hao walivamia eneo la Engaruka.