Operesheni maalumu ya Polisi Tanga yanasa 69
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Almachius Mchunguzi akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Picha na Mbonea Herman
Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoani Tanga limeeleza kuwa watuhumiwa waliokamatwa ni wa makosa mbalimbali wakiwemo vishandu, wahusika wa dawa za kulevya na ulaghai wa mtandao.
Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewakamata watuhumiwa 69 wanaohusishwa na makosa mbalimbali baada ya kufanya operesheni maalumu katika maeneo tofauti ya mkoa huo.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga aliyoitoa Ijumaa Aprili 24, 2026 imeeleza kuwa watuhumiwa hao wanatuhumiwa kwa makosa ya wizi, uporaji wa simu, uvunjaji wa nyumba, fujo pamoja na udanganyifu kupitia mitandao.
“Operesheni hizi zina lengo la kukomesha vitendo vya uhalifu na kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaimarika muda wote,” amesema Kamanda huyo.
Katika operesheni hiyo pia, mtuhumiwa mmoja alikamatwa akiwa na katoni 46 za pombe bandia aina ya Good Life pamoja na vifaa vya kughushi, huku wengine wakinaswa na dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi katika maeneo tofauti ya mkoa huo.
Aidha, watuhumiwa tisa wamekamatwa kwa kujihusisha na ulaghai wa mtandao kupitia mfumo unaojulikana kama Q-NET na tayari wamefikishwa mahakamani ambapo mashauri yao yanaendelea kusikilizwa.
“Hatua kali za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa wote waliokamatwa,” amesisitiza.
Pia, kundi la watuhumiwa 16 maarufu kama vishandu limekamatwa kwa tuhuma za uporaji na wizi wa simu, ambapo walikutwa na pikipiki 26, nyingi zikiwa hazina namba za usajili huku baadhi zikithibitika kuwa za wizi.
Katika operesheni za kupambana na dawa za kulevya zilizofanyika kuanzia Machi hadi Aprili 2026, jumla ya watuhumiwa 26 walikamatwa, hatua inayodhihirisha juhudi zinazoendelea za kukabiliana na biashara hiyo haramu.
“Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yataendelea kufanyika bila kuchoka,” ameongeza
Kwa upande wa usalama barabarani, madereva 911 walikamatwa kwa kukiuka sheria mbalimbali za barabarani na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.
Katika hatua nyingine, mahakama imewahukumu washitakiwa 12 kwa makosa mbalimbali ikiwemo wizi, kumiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na kutoa taarifa za uongo, ambapo wamepewa adhabu tofauti ikiwemo vifungo gerezani.
“Ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha uhalifu unatokomezwa kabisa,” amehitimisha Kamanda huyo.