OSHA yaweka nguvu kuboresha miundombinu shule ya Kambangwa
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akiwasilisha hotuba yake wakati wa Mahafali ya 26 ya Kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Kambangwa akiwa ni mgeni rasmi wa mahafali hayo yaliyofanyika leo Septemba 5, 2025.
Muktasari:
- Shule ya Sekondari Kambangwa ilianzishwa Julai, 1997 na kuzinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin WMkapa na inahudumia zaidi ya wanafunzi 1,300
Dar es Salaam. Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeahidi kuiwezesha Shule ya Sekondari Kambangwa Dar es Salaam kwa kuipatia vifaa muhimu vya kujifunzia zikiwemo kompyuta, kichapishi (printer) pamoja na kujenga uzio wa shule hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa Septemba 4,2025 na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda wakati akihutubia katika Mahafali ya 26 ya kidato cha nne ya shule hiyo ambapo alialikwa kama mgeni rasmi.
Mahafali hayo yaliyofanyika katika viunga vya shule hiyo, yalianza kwa shamra shamra za kuwapongeza wahitimu zilizojumuisha burudani na maonesho mbalimbali ya kitaaluma na kisha kufuatiwa na risala ya wahitimu pamoja na taarifa ya shule iliyowasilishwa na Mkuu wa shule, Angelina Mwakalukila.
“Tunaishukuru Serikali yetu kwa kugharamiwa masomo ya vijana wetu kupitia sera ya elimu bila malipo ikiwemo kutupatia vitabu vingi vya masomo ya sayansi vinavyoendana na sera ya ufundishaji wa mtaala mpya. Kwasasa hatuna upungufu wa vitabu,” amesema.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kambangwa.
Kupitia risala yake, mkuu huyo wa shule ameongezeka kuwa:“Ndugu Mgeni Rasmi palipo na mafanikio hapakosi changamoto kadhalika shule yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maktaba, kompyuta, kuchakaa kwa baadhi ya miundombinu ya madarasa pamoja na shule kushindwa kukamilisha ujenzi wa uzio wa shule.”
Akiwasilisha hotuba yake katika mahafali hayo,Mwenda ambaye ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, amewapongeza wahitimu kwa kufikia hatua hiyo muhimu.
Aidha, amewapongeza walimu, wazazi na walezi kwa kushirikiana kuwalea vizuri wanafunzi hao huku akiwasisitiza kujiandaa kikamilifu kwa mitihani yao mwisho itakayofanyika kuanzia mwezi ujao.
“Ninaungana na wazazi na walimu kuwatakia kila la heri katika mitihani yenu na inshallah Mwenyezi Mungu atawaongoza kufanya vizuri ili muweze kutimiza ndoto zenu.
Vile vile, natambua kwamba baadhi yenu mmefikia umri wa kupiga kura hivyo nitumie fursa hii kuwakumbusha na kuwahimiza kushiriki zoezi la kupiga kura ifikapo Oktoba 29 ili nchi yetu iweze kupata viongozi bora,”amesema.
Aidha, ameahidi kushirikiana na uongozi wa shule kutatua changamoto mbali mbali zilizowasilishwa na Mkuu wa Shule kupitia program ya kusaidia jamii (CSR programme) ya Taasisi yake.
“Serikali imetuagiza kutenga fedha kwa ajili ya kuchangia utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii ambapo Taasisi ya OSHA kupitia sera yake ya kusaidia jamii, tutaisaidia shule hii kukamilisha ujenzi wa uzio pamoja na kuwanunulia kompyuta 10 na vichapishi (printers),” ameongeza.