Padri soka mgonjwa, kesi yaahirishwa

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi na Mahakama ya Wilaya Moshi zimeahirisha kesi za ubakaji zinazomkabili Padri Sostenes Soka wa Kanisa Katoliki Parokia Teule ya Mtakatifu Deonis Aropagita hadi Oktoba 25 kwa madai ni mgonjwa.


Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi na Mahakama ya Wilaya Moshi zimeahirisha kesi za ubakaji zinazomkabili Padri Sostenes Soka wa Kanisa Katoliki Parokia Teule ya Mtakatifu Deonis Aropagita hadi Oktoba 25 kwa madai ni mgonjwa.

Leo Jumatano Oktoba 12, 2022 kesi moja ya ubakaji namba 45 ya mwaka 2022 imetajwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha kwa ajili ya kuanza kusikilizwa

Katika kesi hiyo, mshtakiwa anakabiliwa na shitaka la kumbaka mtoto (12), Agosti 12, 2022 ambapo siku ya tukio mtoto huyo alikua akishiriki mafundisho ya kipaimara katika kanisa hilo lililopo barabara ya Kawawa, Uchira.

Wakili wa Serikali Kasimu Nasiri akiongozana na Sabitina Mcharo wamedai kuwa mtuhumiwa hakufika mahakamani hapo leo.

Wakili wa Utetezi, Edwin Silayo aliileza mahakama hiyo kuwa mteja wake ni mgonjwa, na amelazwa katika hospitali ya kibosho anakoendelea kupatiwa matibabu na kuiomba mahakama hiyo kuwapa tarehe nyingine.

Hakimu mshasha ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 25 , 2022