Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi Kilimanjaro wanasa 138, mmoja ahukumiwa kifo

Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Kilimankaro, Simon Maigwa wakati  akitoa ripoti ya matukio ya uhalifu

Muktasari:

  • Aliyenyongwa alipatikana na hatia ya mauaji.

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewatia mbaroni watu 138 wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya jinai, ikiwemo ujangili na biashara ya dawa za kulevya, katika operesheni maalumu iliyoanza Mei mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo leo Juni 16, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema hali ya ulinzi na usalama mkoani humo imeendelea kuwa shwari, huku kikiwemo mkakati endelevu wa kusaka wahalifu.

Kamanda Maigwa amesema katika mtandao wa dawa za kulevya, watuhumiwa 67 walinaswa ambapo kati yao 25 walikutwa na kilo 21.14 za bangi, huku wengine 42 wakipatikana na kilo 235.14 za mirungi.

Kuhusu mapambano dhidi ya unywaji na utengenezaji wa pombe haramu ya gongo, Kamanda Maigwa amebainisha kuwa watuhumiwa 54 walikamatwa wakiwa na lita 220.13 za pombe hiyo pamoja na mitambo saba ya kufanyia uchenjuaji.

Katika sekta ya maliasili na utalii, jeshi hilo liliwatia mbaroni watu watatu wakiwa na kilo 55 za nyama ya wanyamapori aina ya tembo na swala, huku wengine sita wakinaswa kwa makosa ya kusafirisha mazao ya misitu kinyume cha sheria.

Silaha zilizokamatwa katika msako huo ni pamoja na bastola, bunduki aina ya Mark IV, shotgun, pamoja na risasi 38.

Katika tukio jingine, watuhumiwa watatu walinaswa wakiwa na kilo 500 za nyavu haramu za uvuvi zenye thamani ya Sh5 milioni.

"Operesheni hizi zinaendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa na zimefanikisha kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha usalama wa wananchi na mali zao," amesisitiza Kamanda Maigwa.

Akizungumzia hatua za kisheria, Kamanda Maigwa amesema baadhi ya watuhumiwa wameshafikishwa mahakamani na kesi 55 zimeshatolewa uamuzi, ikiwemo ya aliyehukumiwa adhabu ya kifo baada ya kupatikana na hatia ya mauaji, huku mwingine akihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji.

Kesi nyingine 50 zilizosalia zilimalizika kwa watuhumiwa kupewa vifungo vya chini ya miaka mitano gerezani au kutozwa faini kulingana na uzito wa makosa yao.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuzuia uhalifu kabla haujatokea.