Polisi kujengewa uwezo upelelezi makosa ya uwindaji haramu

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai

Muktasari:

  • Kutoka kubadilika kwa mbinu za uharamia wa wanyamapori, Jeshi la Polisi limesema litaanzisha mtaala maalumu utakaohusu upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ya kesi zinazohusiana na uwindaji haramu wa wanyama pori ili kuwajengea uwezo askari wanaopita katika vyuo vya jeshi hilo.


Moshi. Kutoka kubadilika kwa mbinu za uharamia wa wanyamapori, Jeshi la Polisi limesema litaanzisha mtaala maalumu utakaohusu upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ya kesi zinazohusiana na uwindaji haramu wa wanyama pori ili kuwajengea uwezo askari wanaopita katika vyuo vya jeshi hilo.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai ameeleza hayo leo Oktoba 11, 2022 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wakufunzi 120 wa vyuo vya polisi yaliyoandaliwa na shirika la Traffic International na kufanyika mkoani Kilimanjaro.

Kingai amesema lengo ni wakufunzi hao kufikisha elimu ya namna ya kufanya upelelezi na kuendesha mashtaka ya kesi zinazohusiana na uwindaji haramu wa wanyamapori wataifikisha elimu hiyo kwa askari wote wanaopita katika vyuo hivyo.

"Mafunzo haya yataongeza ufanisi kwa askari wetu katika kukabiliana na uwindaji haramu wa wanyama pori na maliasili zetu," amesema Kingai.

Amesema usalama katika hifadhi umeongezeka ambapo kwa siku za hivi karibuni hakuna matukio ya kihalifu yaliyotendeka tofauti na siku za nyuma ambapo kila siku yaliripotiwa matukio mengi.

Kwa upande wake, Dk Andimile Martini kutoka Traffic International amesema kuwa biashara ya wanyamapori inafanyika katika hifadhi na hufanywa na makundi mbalimbali ikiwamo wawindaji ambao mara nyingi huishi karibu na hifadhi, makundi ambayo wananunua na makundi ya walaji.

Amefafanua kuwa utafiti umebaini kuwa ujangili ni tishio kubwa kwa wanyama pori ambapo kumekua na uelewa mdogo juu ya athari za uwindaji haramu.

Naye William Mallya ambaye ni meneja wa mradi huo amesema kuwa  mradi umelenga kutoa mafunzo kwa waalimu wa vyuo vya polisi Tanzania ambavyo ni pamoja na Chuo cha Polisi Moshi, Chuo cha Polisi Dar es salaam na Chuo cha polisi  Zanzibar, lengo likiwa ni kahakikisha wakufunzi wanakuwa na uelewa kwa ajili ya kuwafundisha askari wanaopita katika vyuo hivyo.

Kwa upande wake, mkufunzi kutoka chuo cha Polisi Moshi, Julius Majura amesema kuwa changamoto kubwa katika kukabiliana na ujangili ni kukosekana kwa taaluma maalumu ya uendeshaji wa upelelezi na mashtaka.

Amesema baada ya mafunzo hayo, wanatarajia kupata ujuzi utakaowezesha kupunguza kukomesha kabisa uwindaji haramu wa wanyama pori.