Polisi Mbeya yawashikilia 871 kwa tuhuma za uhalifu, wamo wa mauaji
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake
Muktasari:
- Watuhumiwa hao walikamatwa kwenye doria zilizofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, kati ya Mei Mosi hadi 31, 2026.
Mbeya. Watu 871 wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma mbalimbali ikiwepo mauaji, kujeruhi, kubaka na kupatikana na dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amewaambia waandishi wa habari leo Juni 4, 2026 katika taarifa yake ya kipindi cha Mei.
Kuzaga amesema kwa kipindi cha Mei Mosi hadi 31, 2026, Jeshi la Polisi lilifanya doria na kubaini watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya uhalifu.
Amesema miongoni mwa watuhumiwa hao, wapo waliohusisha na matukio ya mauaji, ubakaji, kujeruhi, kupatikana na silaha, dawa za kulevya na wizi.
“Kati ya watuhumiwa 871, wapo ambao upelelezi wa kesi zao ulikamilika na kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia na kuhukumiwa kutumikia kifungo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kuzaga amesema wanamshikilia Baraka Mwakatoke (31) na Said Baraka (39), wakazi wa Dodoma, kwa tuhuma za kupatikana na vipodozi vyenye viambata vyenye sumu vilivyopigwa marufuku kuingizwa nchini.
Kuzaga amesema watuhumiwa hao walikamatwa Mei 28, 2026 saa 8:30 usiku katika kizuizi cha eneo la Chimala, Wilaya ya Mbarali katika barabara kuu ya Njombe – Mbeya.
Amesema watuhumiwa walikamatwa na shehena na vipodozi boksi 403 ambavyo walikuwa wakisafirisha kutoka Tunduma, Mkoa wa Songwe kwenda Dodoma.
“Lakini pia walikamatwa na vitenge jozi tatu ambazo ziliingizwa nchini bila kulipia ushuru wa forodha, upelelezi unaendelea ili wafikishwe mahakamani,” amesema.
Wakati huohuo, Kuzaga amesema wanamshikilia Shaban Safari (48), mkazi wa Kyela mkoani Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na kete 27 za dawa za kulevya aina ya heroini.
Kuzaga amesema mtuhumiwa alikamatwa Juni 2, 2026 katika Mtaa wa Roma Kata ya Kyela Kati, Tarafa ya Unyakyusa mkoani Mbeya, akiwa na dawa hizo pamoja na bangi yenye uzito wa gramu mbili.
“Uchunguzi umebaini mtuhumiwa ni muuzaji wa dawa hizo za kulevya na kwamba upelelezi wa kina unaendelea ili afikishwe mahakamani,” amesema.
Akizungumzia jambo hilo, mkazi wa Kabwe jijini Mbeya ameomba Jeshi la Polisi kudhibiti uuzwaji na matumizi ya dawa za kulevya kufuatia kuwepo kwa athari kubwa kwa vijana ambao ni Taifa la kesho,” amesema.