Polisi na kampeni kupinga ukatili wa kijinsia, unyanyasaji watoto
Muktasari:
- Kampeni hiyo imezinduliwa leo Jumatano Agosti 28, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin kuzaga yenye kaulimbiu ‘Tuwaambia kabla hawajaharibika.’
Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeanza kampeni ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto sambamba na kuhimiza wazazi na walezi kutekeleza majukumu yao ya kuwalinda.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Agosti 28, 2024 kuhusiana na kampeni hiyo iliyozinduliwa katika Shule ya Sekondari Mbeya Day, Kamanda Kuzaga inalenga kutoa elimu kwa wanafunzi shuleni.
Amesema wanawaambia wasikubali kurubuniwa na kufumbia macho vitendo vya ukatili ambavyo vinakatisha ndoto zao za maisha yao na badala yake kuwafichua.
"Ni vyema watoto wakapewa ulinzi kuanzia ngazi ya familia kupitia kwa wazazi, jamii, walezi na viongozi wa dini sambamba na kuwapa wigo wa kutoa taarifa za siri za viashiria vya vitendo vya ukatili wa kijinsia ili hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema kamanda huyo.
Msaidizi wa Dawati la Jinsia na Watoto, Mkaguzi wa Polisi, Loveness Mtemi amewakumbusha wanafunzi majukumu yao ni kupata elimu na kuwataka kuongeza juhudi katika masomo na waepuka vishawishi.
"Jukumu lenu ninyi kama wanafunzi kusoma ili kutimiza ndoto za maisha ya baadaye na kutoa ushirikiano wa watu ambao wanajihusisha kuwarubuni ili sheria ifuate mkondo wake" amesema Mtemi.
Mkuu wa Dawati la Jinsia la Watoto Mkoa wa Mbeya, Mrakibu msaidizi wa Polisi, Veronica Ponera amewaonya wanafunzi kutojihusisha na vitendo vya ubakaji, ulawiti na kuingiliwa kinyume na maumbile.
Mkuu wa shule hiyo, Francis Mwakihaba amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuwajengea uwezo vijana na kuomba elimu hiyo iwe endelevu ili kusaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kutamaliki kila kukicha.