Polisi waikamata Hiace iliyojaza wanafunzi Iringa
Gari lililokuwa limepakia wanafunzi 33 mkoani Iringa wakati uwezo wake ni kubeba wanafunzi kati ya 10 hadi 12.
Muktasari:
Wakati Kikosi cha Usalama Barabarani kikiendelea na misako mbalimbali inayosaidia kupunguza ajali za barabarani, mkuu wa kikosi hicho Mkoani Iringa, Mosi Ndozero amekamata gari aina ya Toyota Hiace lililokuwa limejaza wanafunzi 33 wakati uwezo wake ni kubeba abiria 12 tu.
Iringa. Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Iringa, Mosi Ndozero amekamata gari aina ya Toyota Hiace lililokuwa llimejaza wanafunzi 33 wanaosoma katika shule za msingi tatu za Ummusalama, Gangilonga na Mapinduzi mjini Iringa na hivyo kuhatarisha usalama wao.
Kutokana na hali hiyo licha ya kumshikilia dereva wa gari hilo, ameagiza wazazi na walezi wa watoto hao kuchukuliwa hatua za kisheria ili liwe fundisho kwa wazazi wengine wanaoruhusu watoto kurundikana kwenye magari za shule kinyume cha taratibu na sheria.
Akizungumza na Mwananchi, Ndozero amesema wanafunzi wanapokuwa kwenye vyombo vya usafiri ni abiria kama walivyo abiria wengine hivyo wanayo haki ya kukaa kwenye siti na sio kupakatana jambo linalohatarisha usalama wao.
“Uwezo wa ile gali ni kubeba abiria 12 tu lakini watoto walijazana kiasi cha kukosa hata hewa, hii sio sawa kabisa na kamwe hatuwezi kuruhusu hali hii hata kidogo.
“Nasikitika kuona tunao wazazi ambao hawajui hali wala wajibu wao kwa watoto wao, wanachofanya wao ni kupakia tu watoto kwenye gari bila kujali usalama wala wanasafirije,” amesema.
Ameagiza wazazi na walezi wote kuhakikisha watoto wao wanapanda usafiri bora huku akiwaagiza madereva wanaoendesha magari ya shule kusingatia sheria za usalama barabarani.
“Huu tunaita ni ukatikili kwa watoto kwa hiyo wazazi wao watachukuliwa hatua na tutawaelimisha zaidi umuhimu wa kuwahakikishia watoto wao usalama wanapokuwa kwenye vyombo vya usafiri,” amesema.
Amesema kitu kibaya ni kwamba gari inayopakia watoto hao imewekwa vioo vyeusi kiasi kwamba mtoto akifanyiwa ukatili wa kingono hawezi kuonekana nje wala kubainika.
“Marufuku kupakia watoto kwenye magari tinted, watoto wakifanyiwa ukatili humo hata akipiga kelele hakuna mtu wa kumsikia.
“Gari hili ni bovu na wala halina utaratibu wa kuonekana kwamba ni la shule. Rai yangu kwa mkoa wa Iringa kwamba ikiwa kuna wazazi hawajui wajibu wao waanze kuujua tangu sasa,” amesema Ndozero.
Baadhi ya wazazi na walezi waliozungumza na Mwananchi wamesema hawakuwa wakijua kama gari hiyo nyakati za jioni inajaza kiwango cha kushindwa kuwafanya watoto wao wawe hatarini.
“Mimi mwanangu huwa karibia wa mwisho kushuka kwa hiyo sikuwa najua kama anajazwa kwen ye gari kiasi hicho. Tunashukuru kwa gari hili kukamatwa na tunaahidi kuwa makini zaidi,” amesema Huruma Kikoti, Mkazi wa Zizi la Ng’ombe, Manispaa ya Iringa.