Polisi wamfukuza trafiki kwa rushwa ya ngono

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani  Kilimanjaro limemfukuza kazi askari wake wa kikosi cha usalama barabarani kwa tuhuma ya kuomba rushwa ya ngono.

Askari huyo mwenye namba F.4958Cpl, Peter Albert Moshi alinaswa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humu Januari 6 mwaka huu kwa madai ya kuomba rushwa ya ngono kwa mama wa mtoto aliyegongwa na pikipiki ili aweze kumkamilishia taarifa ya uchunguzi wa awali.


Awali askari huyo alikuwa akichunguza ajali ya pikipiki ambayo ilimgonga mtoto wa mama huyo na kusababisha kuvunjika mkono ambapo mpaka sasa anaendelea na matibabu.

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona alisema leo Januari 17, mwaka huu tayari askari huyo wa kikosi cha usalama barabarani ameshachukuliwa hatua za kijeshi ikiwemo kumvua uaskari na kumfukuza kazi.


"Sisi Jeshi la polisi, askari yoyote akikamatwa na kosa la jinai kama hilo na kutakiwa kufikishwa mahakamani lazima tunachukua hatua za kijeshi kwanza ikiwa ni kumvua nafasi yake.

"Tayari sisi tumeshaachana naye na ataendelea kuchunguzwa na tuhuma zinalomkabili, hivyo hatuko naye tena tumeshamfukuza kazi, sasa hatua nyingine za kisheria zitafuata," aliongeza Kamanda Makona.

Taarifa za awali za kiuchunguzi zilizofanywa na Takukuru mkoani hapa zilibaini kuwa askari huyo alikuwa akimsumbua mama huyo kwa muda mrefu na sasa hatua inayotarajiwa kufuata ile ya kupeleka suala hilo mahakamani.