Polisi wamkamata anayedaiwa kumuua dada yake kwa panga
Muktasari:
- Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro linamshikilia Neoni Lazaro(39) mkazi wa Singa Kibosho, wilaya ya Moshi kwa madai ya kumuua dada yake, Magreth Mushi (50) kwa kumkata kata na panga kichwani walipozozana kuhusu mauzo ya nyanya.
Rombo. Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro linamshikilia Neoni Lazaro(39) mkazi wa Singa Kibosho, wilaya ya Moshi kwa tuhuma za kumuua dada yake , Magreth Mushi (50)kwa kumkata kata na panga kichwani walipokuwa wakizozana kuhusu mauzo ya nyanya.
Magreth ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Urauri , kata ya Reha wilayani Rombo alifariki dunia Februari 10 mwaka huu katika Hospitali ya Huruma iliyopo wilayani humo alikokimbizwa kupatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa.
Kaimu Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Ronald Makona amethibitisha leo Februari 14 kukamatwa kwa kijana huyo akisema amekamatiwa jana Wilaya ya Moshi.
"Ni kweli tumemkamata mkazi wa Kijiji cha Singa Kibosho wilaya ya Moshi, Noeni Lazaro kwa kujihusisha na mauaji ya dada yake aliyekuwa akiishi Rombo.Ni yule kijana aliyetoroka baada ya kutekeleza mauaji haya, tumemkamata jana hapa Moshi," amesema Kamanda Makona.
Mwili wa mwanamke huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma iliyopo wilayani humo kwa ajili ya taratibu za mazishi.