Polisi wamshikilia anayedaiwa kubaka, kuua

Polisi wamshikilia anayedaiwa kubaka, kuua

Muktasari:

  • Polisi Mkoa wa Mbeya wanamshikilia mtu mmoja kwa madai ya kuhusika na ubakaji na mauaji ya mtoto mwenye miaka sita.

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Hamis Ibrahim (15) kwa tuhuma za kubaka mtoto wa miaka sita (jina limehifadhiwa), ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza aliyekutwa akiwa amefariki katika jengo lisilokamilika baada ya kufanyiwa ukatili huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 8, 2021, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amesema kuwa marehemu alitoweka nyumbani kwao maeneo ya Kata ya Forest ya zamani, Septemba 6, 2021.

Amesema kuwa mara baada ya kutoonekana nyumbani kwa muda mrefu ndugu na majirani walianza kumtafuta bila mafanikio na jana Jumanne Septemba 7, mwili  wake ulikutwa  umetupwa  kwenye  nyumba hiyo iliyo jirani na maeneo waliyokuwa wakiishi, akiwa amebakwa.

"Baada ya polisi kupata taarifa na kufika eneo hilo, walianza uchunguzi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Kadege katika kata hiyo ya Forest jijini hapa," amesema.

Kamanda Matei amesema kuwa Polisi wanaendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa uchunguzi zaidi na ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika Hosptali ya Rufaa Kanda.

Wananchi wa Kata ya Forest Jijini hapa wamelaani vikali kitendo hicho na kuomba vyombo vya dola kutenda haki,.

Diwani wa kata ya Forest, Henry Mwangambako, amekiri tukio hilo kutokea katika kata yake na kulishukuru Jeshi la Polisi kuwahi kufika eneo la tukio mara baada ya kupata taarifa na kuuchukua mwili wa marehemu.