Presha ya uchaguzi yaanza kupanda

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Dar es Salaam. Ulikuwa mjadala wa kupeana ‘makavu’ kwenye mkutano wa wadau wa siasa nchini kuhusu hali ya demokrasia, hali iliyoonyesha wazi kuwepo presha ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu 2025.

Katika mkutano huo ulioanza Agosti 22, 2023 ma kuhitimishwa jana Agosti 23, 2023  hoja nyingi zilielekezwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM-Bara), Abdulrahman Kinana aliyekuwepo kukiwakilisha chama hicho.

Miongoni mwa hoja hizo ni madai kuwa CCM ndiyo sababu ya kudorora kwa mchakato wa Katiba mpya na wengine wakitaka hakikisho la kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya uchaguzi unaofuata.

Akizungumzia suala hilo lililoibuliwa na wadau kwa namna tofauti, Kinana alisema si ajabu kwa CCM kutajwa kuhusu hayo kwa kuwa ndiyo inayoshika dola, ndiyo yenye Serikali na ndiyo chama kinachotawala, hivyo hakina namna ya kukwepa tuhuma hizo.

Ingawa hakuwa na hakikisho, Kinana alieleza matumaini yake kwamba Tanzania itakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu 2025 ikiwa na muafaka wa tume huru na wa haki.

"Baada ya Rais (Samia Suluhu Hassan) kutoa kauli nyingi sana juu ya dhamira yake ya Katiba mpya, maridhiano na R4 zake, mimi naamini kwamba tutakwenda kwenye uchaguzi wa 2024 na 2025 tukiwa na muafaka wa jumla na maelewano yanayokidhi uchaguzi huru na wa haki," alisema.

Aliunganisha majibu hayo na hoja ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliyesema ni vigumu kubadilisha sheria za uchaguzi bila kufanya mabadiliko ya sheria mama ambayo ni Katiba.

Mnyika alisema baadhi ya sheria za uchaguzi mabadiliko yake yanagusa vifungu vya Katiba, hivyo haitawezekana kuvibadili bila kupeleka bungeni muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba.

Alisema muswada huo ndio utakaoruhusu kufutwa au kubadilishwa kwa vifungu husika katika Katiba.

"Nasisitiza kwamba ni vigumu kujihusisha na mabadiliko ya sheria za uchaguzi bila kuanza na mabadiliko ya Katiba ama kwa ujumla wake au marekebisho ya baadhi ya vifungu (vya Katiba)," alisema Mnyika

Kuhusu hilo, Kinana alisema haamini kuwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi yanahitaji kwanza, mabadiliko ya Katiba.

Katika eneo hilo la Katiba, Msemaji wa CUF, Mohammed Ngulangwa aliituhumu CCM kuwa ndiyo iliyosababisha mkwamo katika mchakato wa Katiba wa mwaka 2014.

Hilo lilimuibua Mjumbe wa Kamati ya Utekeleza ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Hawa Ghasia aliyeeleza kushangazwa na madai dhidi ya chama hicho kuwa kiliukwamisha mchakato huo.

Ghasia, aliyewahi kuwa mbunge na waziri alisema CCM ndiyo iliyoonyesha utashi wa kuridhia mchakato huo na kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini baadaye vyama vya upinzani vikasusia vikao wakati wa hitimisho.

"Wenzetu mliamua kuacha kipindi ambacho tayari dereva ameshapatikana na gari imeanza kutembea, leo hii kama CCM inataka huo uharaka ingeshafanya kwa sababu ina nguvu ya kuamua, lakini hekima za Rais Samia ndizo zinazofanya mambo yaende hivi vizuri," alisema.

Kauli ya Ghasia ilimnyanyua Juma Duni Haji, mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, akisema sababu za upinzani kususia mchakato wa Katiba Mpya 2014, ni hatua ya CCM kwenda na Katiba iliyotoka mifukoni mwao.

"Hatukukimbia mchakato, tuliondoka baada ya kuona mnataka kutuletea Katiba yenu kutoka mifukoni, siyo ile wananchi wanayoihitaji," alisema Duni.

Maoni mapya

Katika hatua nyingine, Mnyika alieleza kusikitishwa na kutotekelezwa ahadi za Rais Samia kuhusu Katiba mpya, akitolea mfano ya kuundwa kwa kamati za mchakato huo.

“Nisikitike pia, hivi karibuni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ametoa kauli kwamba mchakato utaanza Septemba (mwaka huu) kwa kutoa elimu kwa wananchi, jambo ambalo lilishafanyika, njia hii si sahihi,” alisema Mnyika

Kasoro katika tume

Akichangia mjadala huo, Joseph Selasini, makamu mwenyekiti wa NCCR Mageuzi alizungumzia mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi akisema kwa jinsi ulivyo, uchaguzi unasimamiwa na watu ambao ni makada wa CCM.

“Tumekuwa na chaguzi lakini zimekuwa kama kiinimacho kuonyesha tuna demokrasia, lakini hazibebi utashi wa wananchi,” alisema.

Alisema demokrasia imekuwa ikiingiliwa na wanaoshiriki uchaguzi wanajikuta kwenye mateso ya vipigo kutoka kwa vyombo vya dola.

“Hatuwezi tukaingia kwenye uchaguzi, chama fulani kina mabilioni ya fedha, kingine kina mamilioni ya fedha alafu kuna ambacho hakina kitu kabisa,” alisema.

Vilevile, mbunge huyo wa zamani wa Rombo alisema ni igumu kuzungumzia demokrasia ilhali vipo baadhi ya vyama visivyo na uwezo wa kufanya safari hata ya kilomita chache kuelimisha jamii kuhusu demokrasia.

“Watu wengi wana uwezo wa uongozi, lakini wanashindwa kuingia kwa sababu hawamudu gharama za kutafuta uongozi, tukifanya hivi tutaendelea kuwa na viongozi matajiri na wale wengine watabaki kama walivyo,” alieleza.

Selasini alisema kinachotakiwa ni Tume huru, kwa maana ya mlolongo mzima wa tume kuanzia juu hadi chini.

Alipendekeza kiwepo chombo huru kitakachopendekeza kwa njia ya mahojiano, watu ambao Rais atawateua kuunda tume.

Baada ya kuteuliwa, alishauri watu hao ndio wanapaswa kuandika kwamba nani anatakiwa awe msimamizi wa uchaguzi eneo fulani na watakaotajwa waajiriwe kuifanya kazi hiyo.

“Tunapozungumza uchaguzi mkuu mwanzo wake ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hausimamiwi na sheria za uchaguzi bali unasimamiwa na Tamisemi,” alisema.
Demokrasia ndogo

Katika mjadala huo, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji alisema iwapo ataulizwa kuwa Tanzania ina demokrasia au la, atajibu iliyopo ni ndogo mno.

“Tatizo tulilonalo ni kwamba demokrasia yetu imemilikiwa na dola, tunaitazama CCM lakini hata yenyewe ingekuwa kama sisi tuko madarakani, ingelalamika,” alisema.

Alieleza vigezo vya demokrasia ni watu kuwa huru, kuwa na Serikali iliyochaguliwa na watu kwa ajili ya watu na kuwepo vyombo vinavyolinda uhuru wa watu.

“Hatujawa huru kuichagua Serikali tunayoitaka, bahati mbaya sheria tumetunga wenyewe na Katiba tumetunga wenyewe lakini hatuzifuati,” alisema.

Alieleza kama Tanzania ipo tayari kuwa na demokrasia, sheria zilizotungwa kuendesha uchaguzi zinapaswa kufuatwa.

“Hivi sasa bado sheria zetu, angalau mwaka huu zimalizike ili angalau itakapotoka uchaguzi wa Serikali za Mitaa tuwe na uchaguzi huru,” alieleza.

Hata hivyo, alisema tatizo la Tanzania ni kukosekana utashi wa kisiasa, kwani makongamano lukuki yanafanyika bila utekelezwaji.

“CCM tangu mwanzo hawakuwa wanataka vyama vingi na muda wote wanasimama kuhakikisha CCM inabaki madarakani,” alisema.

Alieleza kama taratibu zitafuatwa inawezekana kwa wawakilishi wa vyama vyote vya siasa nchini wawepo bungeni.

Cheyo aivaa Chadema

Alipopewa nafasi ya kuzungumza, mwanasiasa mkongwe, John Cheyo alielekeza hoja yake kwa Mnyika, akimwambia hakuna faida ya kususia mambo yenye masilahi ya kitaifa.

Alitaka utamaduni wa kususia kila kitu uachwe, akisema hauipeleki nchi popote.

"Nchi hii ni yetu wote, si ya chama kimoja ni yetu wote, yakiharibika hapa hakuna pa kukimbilia," alisema Cheyo, maarufu kama Mzee Mapesa.

Hoja ya Rungwe

Mengine yaliyozungumzwa ni kuhusu uhuru wa maoni, hoja iliyoibuliwa na Mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe aliyesema uliopo una mipaka.

"Binadamu kama hatakuwa na uhuru wa kuzungumza ujue ni matatizo katika jamii yenu ama nyumbani au katika taifa, lakini binadamu ameumbwa ili awe na fikra," alisema.

Alieleza kila mtu anapaswa awe na uhuru wa kuzungumza isipokuwa asikiuke mipaka, mathalan kutoa lugha za matusi.

Kwa mujibu wa Rungwe, wananchi wa Tanzania wamekuwa na woga wa kuzungumza wakidhani watafuatwa na vyombo vya dola, hivyo uhuru walionao umekuwa na mipaka.

"Uhuru huu una mipaka yake, nimetoa kama ufupisho, lakini nafikiri Watanzania kwa ujumla wetu tuna haki ya kuzungumza hasa mambo yanayotukera, lazima uzungumze ili Serikali itusikie," alisema.

Katika hilo, Selasini alisema uhuru unapaswa kuwa na mipaka, hasa ya kuzingatia tunu za taifa.

Pamoja na kuwepo uhuru, hakupaswi kutolewa lugha chafu na matusi dhidi ya wanasiasa majukwaani.

"Ikitokea mwanasiasa mmoja amemwambia mwingine kwamba mwenyekiti wa chama fulani ni mjinga, unadhani anasababisha nini kwa wafuasi wa chama hicho, tuwe na lugha nzuri," alisema.