Profesa aomba kura akatatue changamoto za walima korosho

Muktasari:

Mgombea Urais CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amewaahidi wananchi wa Tunduru kumaliza changamoto zinazowakabili wakulima wa korosho ikiwa ni pamoja na masoko pamoja na bei endapo watamchagua kuwa Rais wao.

Tunduru. Mgombea Urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amewaomba wananchi wa Tunduru, Mkoani Ruvuma wampigie kura nyingi za ndiyo Oktoba 28 mwaka huu, awe Rais wa Tanzania pamoja na mambo mengine, akamalize changamoto  zinazowakabili wakulima wa korosho nchini humo.

Amesema wakulima wengi wa korosho wanakabiliwa na changamoto ya masoko ya uhakika na upatikanaji wa bei inayouzwa kwenye soko la dunia.

Mgombea urais huyo ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 18, 2020 alipozungumza asubuhi hii na wakazi wa Kata ya Nakapanya, Jimbo la Tunduru Kaskazini.

Profesa Lipumba ambaye yuko njiani kuelekea Wilayani Masasi kisha Mtwara, alisimama Nakapanya kwa lengo la  kumnadi diwani wa kata hiyo.

“Bado bei ya masoko ya uhakika kwa wakulima ni changamoto hawapati bei inayopatikana kwenye masoko ya dunia, tunaomba mtuchague tuweze kuliasisi zao hili la korosho hapa Tunduru,” amesema Lipumba.

Amesema nchi inahitaji kila mkulima awe na haki ya kuuza korosho kwa mnunuzi yeyote atakayetoa bei kubwa yenye faida kwake.

“Tunahitaji mkulima awe na haki ya kuuza korosho zake kwa mtu atakayempa bei kubwa zaidi na sio kupangiwa bei ya kuuza korosho, tunataka kuwe na ushindani wa kununua korosho kwani zina bei kubwa duniani," amesema.

Amesema Tanzania inataka wafanyabiashara washindane kwa kutoa bei kubwa kwa wakulima ili wanufaike na zao hili la korosho.

“Tunaomba kura zenu Oktoba 28 tukasimamie haya ili muweze kunufaika na kilimo hiki,” amesema Profesa Lipumba.