Profesa Baregu afariki dunia

Muktasari:

  • Aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema Profesa Mwesiga Baregu amefariki dunia.

Dar es Salaam. Mwanachama wa Chadema na mwanazuoni, Profesa Mwesiga Baregu amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili Juni 13, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

 Mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma Muhimbili, Aminiel Aligaesha  amesema, “amefariki saa tano usiku wa kuamkia leo akiwa ICU (chumba cha uangalizi maalum)  na alikuwa hapo kwa takribani siku 15.”

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mkurugenzi wa Itikadi na Uhusiano wa kimataifa wa Chadema, John Mrema amesema chama kitatoa taarifa rasmi taarifa baada ya kikao na wanafamilia.

"Tunaelekea hospitali ya Muhimbili kukutana na wanafamilia halafu tutatoa taarifa rasmi," amesema Mrema.

Katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter  Waziri wa Viwanda na Biashara,  Profesa Kitila Mkumbo amesema, "pumzika kwa amani Profesa Baregu. Mmoja wa wasomi walioamini kuwa huwezi kutenganisha taaluma na siasa. Ulitufundisha baadhi yetu tunaokubali msimamo huo wasomi wanaweza kufanya siasa bila kupoteza sifa zao.’”

Mwingine aliyeandika ujumbe Twitter ni  kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akimtakia mapumziko mema Profesa Baregu.

Profesa Baregu aliyekuwa mhadhiri wa sayansi ya siasa na utawala wa umma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baadaye alisitishiwa mkataba wake kwa kile kilichoelezwa kuchanganya utumishi na siasa.

Baadaye alihamia Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema hadi mwaka 2019.