Profesa Mbarawa: Mkataba huu hauna maeneo yanayoifunga Serikali

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano undani wa mkataba wa makubaliano (IGA) kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, akisema kuwa mkataba huo hauna masharti yanayoifunga Serikali.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano undani wa mkataba wa makubaliano (IGA) kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, akisema kuwa mkataba huo hauna masharti yanayoifunga Serikali.

Profesa Mbarawa amebainisha hayo leo Jumamosi Juni 10, 2023 bungeni Dodoma wakati akitoa maelezo kuhusu mkataba huo ambao umeligawa Taifa katika makundi mawili ya wanaoupinga na wanaoutetea mkataba huo.

Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 2 ya mkataba wa IGA, lengo lake ni kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Serikali mbili kwa maeneo mahsusi yaliyoainishwa ndani ya mkataba husika ambayo utekelezaji wake utafanyika kupitia mikataba mahsusi baina ya taasisi zilizoainishwa katika mkataba huo kama taasisi tekelezi ambazo ni mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na DP World.

“Mkataba huu hauna masharti yanayoifunga Serikali kuhusu maeneo ya ushirikiano yaliyoanishwa pasipo uwepo wa mikataba mahsusi wa utekelezaji wa miradi itayojadiliwa na kukubaliwa na pande mbili,” amesema Profesa Mbarawa.

Waziri huyo ameliambia Bunge kwamba, mawanda ya uwekezaji chini ya mkataba huo yatahusisha uendelezaji na uendeshaji wa baadhi ya maeneo ya Bandari na siyo bandari yote kwa ujumla wake.

Pia, amesema uendelezaji na uendeshaji huo utafanyika kupitia mikataba mahsusi ya miradi ambayo itajadiliwa na kuingiwa kwa kila eneo la ushirikiano na itahusisha matumizi ya ardhi pekee na siyo umiliki wa ardhi ikiwa ni pamoja na Serikali kuhakikisha kuwa Sheria, kanuni na taratibu za nchi zinazolinda umiliki ya ardhi ya Watanzania zinazingatiwa na kusimamiwa.

Amesema mkataba huo umeainisha awamu kuu mbili za maeneo ya ushirikiano; awamu ya kwanza itajumuisha: kusimamia, kuendesha na kuendeleza baadhi ya magati katika Bandari ya Dar es Salaam; kuboresha gati la majahazi na gati la abiria katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuvutia vyombo vikubwa zaidi na meli za kitalii kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.

Maeneo mengine, amesema ni kuwekeza katika maeneo yaliyotengwa katika bandari kavu; kufanya uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya Tehama ya kuendeshea shughuli za kibandari ili kuongeza ufanisi wa bandari kuwa shindani; na kuwajengea uwezo watumishi wa TPA.

“Msisitizo wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanabaki chini ya umiliki wa Serikali,” amesema Profesa Mbarawa.