Profesa Mkenda atilia shaka minada ya kahawa
Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizindua bodi hiyo yenye makao makuu Manispaa ya Moshi Mkoani. PICHA| WIZARA YA KILIMO
Muktasari:
- Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda ameitaka bodi ya wakurugenzi wa bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kutathmini wingi wa minada ya kahawa iliyogawanywa katika kanda tatu ili kubaini kama ina tija kwa maendeleo ya zao hilo.
Moshi. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda ameitaka bodi ya wakurugenzi wa bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kutathmini wingi wa minada ya kahawa iliyogawanywa katika kanda tatu ili kubaini kama ina tija kwa maendeleo ya zao hilo.
Ameeleza hayo leo Jumanne Juni 29, 2021 wakati akizindua bodi ya TCB akiitaka kutazama minada ya kahawa ili kuona kama inakidhi matakwa.
Kwa sasa minada ya Kahawa inafanyika Mbinga, Mbozi na Moshi na mwaka 2022 wanakusudia kuanza Kagera.
Profesa Mkenda amesema bodi hiyo inawajibu mkubwa wa kufanya uchunguzi kama kuna tija ya minada hiyo kuwepo katika kanda mbalimbali nchini na kuona kama mkulima ananufaika na minada hiyo au anakandamizwa.
"Mwenyekiti wa bodi na timu yako fanyeni uchunguzi kuhusu minada ya kahawa, kama ina tija kufanyika katika maeneo mengi au inaweza kufanyika mahali pamoja, na mwangalie gharama wanazotumia wanunuzi kwenda kufuata minada katika kanda hizo kama zinamkandamiza mkulima,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuitaka bodi hiyo kutoa elimu juu ya namna minada inavyofanyika ili kujenga uelewa mpana kwa wakulima na wadau wengine wa kahawa ambao hawana uelewa wa minada hiyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TCB, Profesa Aurelia Kamuzora amesema changamoto kubwa inayoikabili sekta ya kahawa ni uelewa mdogo kuhusu zao hilo, na kwamba watashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo wakulima ili kuimarisha na kuboresha zao hilo.