Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Mkumbo ataja maeneo matano kufanikisha Dira ya Taifa 2050

Muktasari:

  • Maeneo hayo ni pamoja na kilimo, mazingira bora ya kufanyia biashara, kukuza pato la taifa, mfumo wa ufuatiliaji na matumizi ya takwimu katika mstari wa Taifa na kimataifa.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imetaja maeneo matano muhimu yatakayowezesha kufikia mafanikio ya Dira ya Taifa 2050 ili kuwapatia Watanzania mafanikio sahihi.

Maeneo hayo ni pamoja na kilimo, mazingira bora ya kufanyia biashara, kukuza pato la Taifa, mfumo wa ufuatiliaji na matumizi ya takwimu katika mstari wa Taifa na kimataifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameliambia Bunge leo Jumanne Juni 23, 2026 wakati akijibu hoja za wabunge zilizoibuliwa wakati wa uchangiaji Mpango wa Taifa na Bajeti ya Serikali 2026/26 ambazo kwa nyakati tofauti viliwasilishwa Juni 11, 2026.

Bajeti hiyo imepitishwa kwa wastani wa asilimia 97.66 ya kura baada ya wabunge 385 kupiga kura ya ndiyo kati ya 393 waliokuwepo bungeni.

Matokeo hayo yametangazwa na Spika wa Bunge, Mussa Zungu kuwa kura nane ziliikataa bajeti hiyo kwa kusema hapana na wabunge wengine wanane hawakuwepo bungeni kwa siku ya leo Jumanne, Juni 23, 2026.

Profesa Mkumbo amesema Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kilimo kinakwenda kuwa mkombozi na kimepewa msukumo kwa ajili ya kufikia malengo hayo, kwani kitasaidia kukuza pato la Taifa kuanzia bajeti ijayo na siku za usoni.

Amesema muundo wa uchumi na nguvu kazi ya nchi ambayo ni asilimia 54.2, vipo kwenye kilimo, mifugo na misitu huku asilimia 10.3 ikiwa ni uzalishaji viwandani wakati asilimia 35.5 ni kwenye sekta ya huduma.

“Utaona asilimia imepungua kwenye kilimo ambayo mwaka 2021 ilikuwa asilimia ni 60.4 2021 lakini sasa ni asilimia 54.2, hii inatarajiwa kupungua kadri uchumi wa kisasa unavyokua na kilimo cha kisasa kinaongezeka. Hii haimaanishi kupungua kwa umuhimu wa kilimo bali ni muhimu kuwa na mizania sahihi katika sekta zote tatu ili kuzalisha ajira kwa wingi,” amesema Profesa Mkumbo.

Waziri pia ameelezea kuhusu mpango na mkakati wa Serikali kwa wafanyabiashara, akisema mazingira bora ya kufanyia biashara ndiyo nyenzo ya kukuza uchumi na kufanya urasimishaji katika mageuzi makubwa ya uchumi, ambayo Tanzania inayalenga.

Alisema bajeti ya Serikali imeweka hatua mahususi za kuchochea sekta ya uzalishaji viwandani ili watu wengi waweze kuajiriwa na huko mbeleni sekta hii itakuwa sekta mama katika ajira.

Waziri huyo amesema katika jitihada za uchumi wa viwanda, kilimo kitaendelea kuwa kipaumbele kikubwa kwa sababu katika mazingira yetu huwezi kuwa na mapinduzi ya viwanda bila kuwa na mapinduzi ya kilimo.

Alitaja eneo jingine kuwa ni sekta isiyo rasmi ambayo Serikali itajielekeza katika kuimarisha ili mchango wake katika uchumi wa Taifa uonekane na kuchangia kutengeneza ajira zenye staha.

Kwenye eneo la kurasimisha sekta isiyo rasmi, amesema mazingira bora ya kufanya biashara yataangaliwa ili iwe rahisi kuanzisha na kufanya biashara, na tayari Serikali imeandaa mkakati mpya wa kuimarisha mazingira ya biashara (Mkumbi 2), hivyo akawaomba wabunge kuunga mkono bajeti kwa kuwa mazingira ya biashara ndiyo yatakuwa nyenzo ya kufanya urasimishaji.

Akizungumzia eneo la pato la Taifa ambalo amesema limekuwa na maswali mengi kwa watu kutokuelewa dhana iliyotumika kwenye mgawanyo, amesema uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2025 ilikuwa Sh234.14 trilioni na pato la taifa kwa kila mtu,  ni pato la taifa lililoganwanywa kulingana na idadi ya watu waliopo nchini.

Eneo la nne ni matumizi ya mstari wa Taifa na kimataifa kwenye kupima umaskini ambapo alisema kiwango cha mstari wa umaskini kilichotumika ni matumizi ya kaya kwa Tanzania bara, ambayo ni Sh63,164 kwa mwezi.

Kwenye maelezo yake, amelitaja jambo la tano kuwa ni mfumo wa ufuatiliaji ambapo amedai Tume ya Taifa ya Mipango imejielekeza kwenye utekelezaji na itapima mafanikio kwa kuzingatia viashiria vya upimaji vinavyozingatia matokeo ya utekelezaji program ya miradi ya maendeleo katika kukuza na uzalishaji.

“Kwa kuzingatia maoni na ushauri wa wabunge Serikali imekubali na tayari imeanza mchakato wa kuandaa sera ya ufuatiliaji na tathmini na muswada wa sheria ya MNE frame work,” amesema Profesa Mkumbo.

Ametaja mikopo iliyotolewa na benki za biashara kwenye shughuli za kiuchumi mwaka 2021 kuwa ilikuwa ni Sh22.44 trilioni wakati kwa sasa imefikia Sh44.60 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 50; huku mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi zilikuwa Dola 6.75 billion na sasa zimepanda na kufikia Dola 10.26 bilioni.

Hata hivyo Waziri Mkumbo amesema ni lazima Watanzania wabadilike na kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali watambue rasilimali kubwa ya kuendeleza nchi ni uwezo wa watu wake na hivyo kuwataka kuunga mkono mpango wa Serikali wa kupanga upya mfumo wa elimu kwa kujikita kutoa watu wenye uwezo badala ya vyeti na sifa za kitaaluma.

Katika hatua zingine, Waziri Mkumbo amezungumzia kauli za aliowaita wapinzani kwamba Serikali ya CCM haina demokrasia, akasema jambo hilo siyo la kweli kwani chama hicho kinaamini katika demokrasia na hata katiba yake imetaja neno haki mara 37.