Rais Mwinyi ateua wengine 14

Tuesday September 14 2021
mwinyipicc

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

By Jesse Mikofu

Unguja. Kasi ya uteuzi wa nafasi mbalimbali za watendaji serikalini inayofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, inazidi kuongezeka baada ya jana kuteua watendaji 14, akiwamo Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Dk Othman Abbas Ali.

Huu ni mwendelezo wa kiongozi huyo kuteua viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali, kutokana na kile alichosema kuwa hata sita kufanya hivyo iwapo ataona kuna sehemu mambo hayaendi sawa.

Kwa kipindi cha takribani wiki moja amefanya teuzi zaidi ya 30 katika nafasi mbalimbali za kiutendaji serikalini.

Hivi karibuni, pia aliwateua makatibu tawala, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa jiji, manispaa na halmashauri za Unguja na Pemba.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, mhandisi Zena Said kwa vyombo vya habari jana, ilisema pia Dk Mwinyi amemteua Juma Yakuti Juma, kuwa Naibu Katibu wa Baraza la Mapinduzi huku Suleiman Ali Suleiman akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Msaidizi wa Baraza la Mapinduzi (sera, ufuatiliaji na tathimini).

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa Yussuf Ibrahim Yussuf, ameteuliwa kuwa kamishna wa idara ya fedha za nje, Saumu Khatib Haji ameteuliwa kuwa kamishna wa idara ya bajeti.

Advertisement

Wengine walioteuliwa ni Haji Ali Haji anayekwenda kuwa mkurugenzi wa idara ya sera za kodi na fedha, huku Suleiman Mohamed Rashid akiteuliwa kuwa mkurugenzi wa idara ya uendeshaji na utumishi.

“Mohamed Hassan Khamis ameteuliwa kuwa Mkurugenzi idara ya mipango sera na utafiti na Siti Abbas Ali, ameteuliwa kuwa kamishina wa idara ya mipango ya kitaifa, maendeleo ya kisekta na kupunguza umasikini,” ilisema taarifa hiyo.

Katika tume ya mipango pia Rais Mwinyi amekugusa baada ya kumteua Ahmed Makame Haji kuwa kamishina wa idara ya ukuzaji uchumi.

Khamis Issa Mohamed anakwenda kuwa ofisa mdhamini, Tume ya Mipango Pemba na Dk Mohamed Juma Abdalla akiteuliwa kuwa katibu mtendaji wa kamishna ya utalii.

Wengine ni Hafsa Hassan Mbamba aliyeteuliwa kuwa mkurugenzi wa idara ya masoko na Aviwa Issa Makame akiteuliwa kuwa mkurugenzi idara ya mipango na maendeleo ya utalii.


Wananchi watoa neno

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi kuhusiana na teuzi hizo walisema huenda bado Rais Mwinyi hajapata watendaji anaowaamini kufanya nao kazi

“Kwa kweli kasi yake ya kuteua ni kubwa mno, itakuwa bado anatafuta watu wenye kasi kubwa kwa ajili ya maendeleo

Mwingine Amisu Saadam alisema: “Watu wengi walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea, sasa wengine wanashindwa kwa hiyo lazima nafasi hizo zijazwe kwa watendaji wanaoweza kukimbia.”

Advertisement