Rais Samia aagiza uchunguzi wa kina, haraka kifo kada wa Chadema
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa pole kwa viongozi wa Chadema na familia ya marehemu Ali Kibao juu ya msiba wa kiongozi huyo wa chama hicho.
Rais Samia ametuma salamu hizo leo Jumapili Septemba 8, 2024 kupitia mitandao yake ya kijamii.
“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa Chadema Bwana Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki.
“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,”ameandika Rais Samia.
Kibao ambaye ni Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema anadaiwa jioni ya Septemba 6, 2024 maeneo ya Kibo Complex Tegeta jijini Dar es Salaam, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga na basi la Tashrif alishushwa kwenye basi hilo na kuchukuliwa na watu wasiojulikana majina yao wala walipotokea.
Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime akizungumza na Mwananchi leo amesema wanafuatilia tukio hilo na wameongeza nguvu kutoka makao makuu.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi mkali na timu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai imetumwa kuongeza nguvu ili kuhakikisha waliofanya mauaji hayo wanapatikana na kufikishwa mahakamani,”amesema Misime.
Endelea kusoma katika tovuti ya Mwananchi