Rais Samia apokea tuzo akimtaja Hayati Magufuli

Wednesday May 25 2022
RAIS PIC1

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022 kutoka kwa Makamu wa Rais wa Sekta Binafsi, Miundombinu na Viwanda kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Solomon Quaynor kwa niaba ya Rais wa Benki hiyo, Dk Akinumwi Adesina.

By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amepewa Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022 (Babacar Ndiaye Trophy 2022) ikiwa ni kutambua jitihada anazozifanya katika ujenzi wa miundombinu nchini.

Tuzo hiyo hutolewa kwa watu mashuhuri duniani ambao wameonyesha dhamira yao ya kuendeleza sekta ya miundombinu ya usafiri.

Mkuu huyo wa nchi amekabidhiwa tuzo hiyo leo Jumatano Mei 25, 2022 katika mkutano mkuu wa mwaka wa 57 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) uliokuwa ukijadili fursa mbalimbali pamoja na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika uliofanyika nchini Ghana akiwa ziarani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema amepokea tuzo hiyo akiwa na hisia mchanganyiko kwa sababu anao uhakika kuwa kwa muda ambao amekaa madarakani usingeweza kumfanya yeye kupata tuzo hiyo.

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa ujenzi wa miundombinu huhitaji muda zaidi kwani kuanzia upembuzi yakinifu unapofanyika hadi fedha zinapopatikana si rahisi kusema ndani ya zaidi ya mwaka mmoja aliokaa angefanikisha.

“Miradi inachukua miaka mingi, ni mchakato endelevu, kwetu sisi ulianzia awamu ya kwanza hadi ya tano mengi yalifanyika ikiwemo kupanua mtandao wa barabara na kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi katika kipindi cha awamu ya Nne kilichoongozwa na Jakaya Kikwete,”

Advertisement
TUZO PIC

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akionyesha Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022 (Babacar Ndiaye Trophy 2022) kutokana na mafanikio kwenye Ujenzi wa Barabara, mara baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo na Makamu wa Rais wa Sekta Binafsi

“Lakini katika jitihada hizi, mtu mmoja alijitokeza ziadi nyakati hizi zote na huyu ni Hayati John Pombe Magufuli (Rais wa awamu ya tano) mtangulizi wangu, alitumika katika awamu ya tatu na nne kama waziri wa ujenzi na uchukuzi kabla ya kuwa kiongozi mkuu wa Taifa ili aendeleza jitihada hizo,”

Alisema anapokea tuzo hiyo huku akiwa haamini kama inaweza kuwa ya mtu binafsi huku akieleza kuwa kama ni ya mtu mmoja basi anayestahili kuliko Watanzania wote ni hayati John Magufuli.

“Ni bahati mbaya hayupo nasi aweze kushuhudia matunda ya jitihada na uongozi wake. Tuzo hii inatupa msukumo viongozi wa Afrika kufanya kazi kuendeleza barabara na reli kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wetu” amesema Samia.

Baadhi ya waliowahi kupata tuzo hizo ni Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari,  Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta huku Rais Samia akiwa Rais wa kwanza mwanamke kupokea tuzo hiyo.

Makamu wa Rais wa Sekta Binafsi, Miundombinu na Viwanda katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Solomon Quaynor amesema ni vyema viongozi wa Afrika kuanza kufikiria kuhusu barabara za kikanda na za ndani kwani kama haiwezekani kuiunganisha Afrika kiuchumi matokeo yanayotafutwa hayawezi kupatikana.

“Tunataka ukanda huru wa biashara wa Afrika uweze kufanya kazi, tumetaja sekta ambazo nazishughulikia, sekta ya viwanda na miundombinu zote tunazishughulikia, siyo tu kufanya biashara kwa ajili ya kusafirisha mizigo lakini pia kuongeza thamani kwa kusaidia viwanda vidogo hasa katika mnyororo wa thamani katika kilimo,” amesema Quaynor.

Advertisement