Rais Samia atengua uteuzi wa Polepole, aondolewa hadhi ya ubalozi
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Hamphrey Polepole.
Muktasari:
- Rais Samia kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma, amemuachisha kazi Polepole kwa manufaa ya umma
Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Dk Samwel Shelukindo imeeleza imepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka ikitaarifu kwamba, Rais Samia Suluhu Hassan kwa mamlaka aliyonayo, ametengua uteuzi wa Humphrey Polepole, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na kumuondolea hadhi ya ubalozi.
Rais Samia kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma, amemuachisha kazi Polepole kwa manufaa ya umma.
Kwa mujibu wa barua hiyo, uamuzi huo umeanza tangu Julai 16, 2025.
Rais Samia amechukua hatua zikiwa zimepita wiki chache tangu Polepole adai kumwandikia barua kumweleza kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu, huku katika barua hiyo aliyoiweka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, akilalamikia baadhi ya mambo.
Katika barua hiyo ya Julai 13, 2025 aliyoiweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, Polepole alieleza kufikia uamuzi huo kwa sababu ya kile alichoeleza ni kusikitishwa na mwelekeo wa uongozi usiojielekeza katika kusimamia haki, amani na kuheshimu watu.
Polepole siyo mtu wa kwanza kuvuliwa ubalozi, wapo mabalozi wengine ambao walivulia hadhi hiyo na marais waliopita.
Polepole amewahi kuhudumu nafasi ya mbunge wa kuteuliwa, mkuu wa wilaya na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM.
Pia, aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba.
Novemba 5, 2018, hayati Rais John Magufuli alitengua uteuzi na kumrejesha nchini Tanzania aliyekuwa Balozi wa Tanzania, Canada, Alphayo Kidata.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati huo, Dk Faraji Mnyepe, uamuzi huo ulianza Novemba 5, 2018.
Dk Mnyepe alisema katika taarifa yake, kwamba Kidata ameondolewa hadhi ya ubalozi.
Mwingine ni Dk Wilbrod Slaa ambaye Septemba mosi, 2023, Rais Samia alimvua hadhi ya ubalozi ikiwa ni takribani miaka sita tangu kuteuliwa kwake, Novemba 2017 kuiwakilisha Tanzania nchini Sweden.
Profesa Costa Mahalu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia uteuzi wake ulitenguliwa na aliondolewa hadhi ya ubalozi lakini baadaye alirejeshewa.