Rais Samia atoa mwelekeo mradi wa Nsongezi, Museveni aomba gesi

Rais Samia Suluhu Hassan akimuonesha kitu Rais wa Uganda, Yoweri Museven wakati wakizindua mradi wa kufua umeme wa Kikagati -Murongo

Muktasari:

Mradi wa Nsongezi ni sehemu ya miradi ya kufua umeme inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Uganda na Tanzania kwa kutumia maji ya Mto Kagera, ambapo utazalisha umeme wa megawati 35 kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili. 

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wataalam katika wizara za kisekta zinazohusika na mradi wa kufua umeme wa Nsongezi kukutana na kujadiliana ili kupata njia bora ya kuutekeleza kwakuwa Tanzania iko tayari kwa mradi huo utakaozalisha megawati 35.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 25, 2023 nchini Uganda wakati akizindua mradi wa kufua umeme wa Kikagati -Murongo pamoja na Rais, Yoweri Museveni wa Uganda, ambapo mradi huo uliogharimu Dola 56 milioni za Marekani utazalisha megawati 14 huku nchi hizo kila moja ikipata megawati saba.

Rais Samia amesema baada ya kukamilika Kikagati-Murongo utakaonufaisha wilaya za Kyerwa, Missenyi na Karagwe mkoani Kagera, Serikali yake iko tayari kwa mradi wa kuzalisha umeme wa Nsongezi utakaozalisha megawati 35 kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda.

“Serikali yangu iko tayari kwa mradi huu na naomba tuwaruhusu wataalam kutoka pande zote mbili kukaa chini kuujadili huu mradi ili kuja na njia bora zaidi ya kuutekeleza,” amesema Rais Samia

Pia, ameahidi kutoa kipaumbele na kuzifanyia kazi kwa haraka baadhi ya changamoto za kisekta zinazoukabili mradi wa Kikagati-Murongo zikiwmo vibali vya Ewura, Mamlaka ya Mapato (TRA), mikataba, vibali vya ajira na makazi ili kuhakikisha mradi huo unafanya kazi kwa ufanisi.

Naye, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema ana matumaini Tanzania itaisaidia nchi yake nishati ya gesi asilia ili kuzalisha chuma, mbolea na matumizi ya nyumbani, huku akieleza kuwa eneo la kijiolojia linazonguka mradi wa Kikagati -Murongo la Ankole -Karagwe linatajwa kuwa na madini sawa na eneo la Katanga nchini Congo (DRC)

“Kwa sasa tunangojea ndugu zetu Watanzania kutukomboa na nishati ya gesi kwa sababu ya kwetu haitoshi na tunahitaji gesi kutengeneza chuma, mbolea, kupikia tunangojea kuinuliwa na ndugu zetu Watanzania, tuliwapelekea mafuta sasa tunangoja gesi, huo ndiyo undugu wa damu,” amesema Museveni

Naye, Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Ruth Nankabirwa amesema megawati 14 zinazozalishwa kwenye mradi huo ni muhimu na nchi yake itaendelea kuhakikisha inazalisha umeme wa kutosha ambapo mradi huo umeweka msingi wa mahusiano mazuri kati ya Uganda na Tanzania.

“Mradi huu unatuma ujumbe kwa bara zima la Afrika kwamba Tanzania na Uganda zinaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana, tunawaomba wananchi wa hapa kulinda miundombinu ya miradi huu tunauacha mikononi mwao na wanapaswa kuhakikisha inakuwa salama na haiharibiwi na watu wenye nia ovu,” amesema