RAS Shinyanga apambana na wizi wa dawa vituoni

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Siza Tumbo.

Muktasari:

  • Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga amewataka wakurugenzi kusimamia afua mbalimbali za mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya ikiwemo kufanya ukaguzi ili kuondokana na wizi wa dawa katika vituo vya afya.

Shinyanga. Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Siza Tumbo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa wa Shinyanga kusimamia kikamilifu afua mbalimbali za mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya.

Tumbo ameagiza wakurugenzi hao kufanya ukaguzi wa dawa ‘Medicine Audit’ mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma, kwa ajili ya kupunguza changamoto zinazotokana na usimamizi mbovu wa bidhaa hizo na kuondokana na wizi wa dawa vituoni.

Hayo ameyasema leo Jumamosi, Machi 18 wakati akifungua mafunzo kwa wakurugenzi wa halmashauri, waganga wakuu wa wilaya, wafamasia na maafisa ugavi wa vifaa vya afya kutoka Halmashauri zote za mkoa wa Shinyanga.

Tumbo amesema kabla ya mfumo  wa mshitiri dawa zilikuwa zikiibiwa sana na zingine kupelekwa kwenye majumba ya watu, lakini kwa sasa mfumo umeboreshwa wizi hautakuwepo tena na atakayepatikana anafanya wizi katika mfumo huo achukuliwe ikibidi kufukuzwa kazi.

"Mlioko kwenye mafunzo haya kila mmoja akatimize wajibu wake, niwaombe mkasimamie ipasavyo na mkahakikishe hizo dawa haziibiwi ili ziweze kufika na kutumika kwenye vituo husika.

“Mkasimamie ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya, ili viweze kulipa washitiri kwa wakati mara baada ya kupokea shehena ya bidhaa, kuepushe madeni yasiyo ya lazima," amesema Tumbo na kuongeza:

"Mtu analipwa mshahara halafu anaiba, hivyo hao watumishi wanatakiwa mkawape elimu na sababu kubwa ya kuleta mfumo huu ni kuondokana na wizi wa dawa, naombeni tubadilike tuwe wazalendo," ameongeza Tumbo.

Aidha amesema kwa kutambua hilo, Serikali imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unakuwa wa asilimia 100 kwa kuweka mfumo wa mshitiri.

Mjumbe wa timu ya uratibu ya mfumo wa mshitiri kutoka ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi) Amiri Mhando, amesema mfumo huo utarahisisha kupatikana kwa huduma za kupata vifaa vya afya kwa wakati na utapunguza upotevu wa dawa.

"Na hii itasaidia kutunza kumbukumbu kwa sababu ya kutumia njia za kielectoniki, tofauti na awali wahusika walikuwa wakisahau kuhifadhi, pia njia hiyo itasaidia kupunguza hoja za ukaguzi na italeta ufanisi kwa kuondoa tatizo la upungufu wa vifaa vya afya na vitafika kwenye vituo kwa wakati," amesema Mhando.

Mfamasia kutoka wilaya ya Ushetu, Alphonce Malunde amesema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa dawa na utarahisisha utunzaji wa kumbukumbu.

Mfamasia kutoka wilaya ya Kishapu, Balungi Samson amesema elimu hiyo wataitumia kwenda kuitoa kwa wahudumu wa afya ili kuondokana na changamoto iliyokuwepo ya mawasiliano ambayo ilikuwa ikitumika kwa muda mrefu.