RC Babu awaasa wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka wajasiriamali mkoani humo, kuzingatia kanuni zote za ubora, usalama wa chakula na mahitaji ya soko ili kuweza kuzalisha bidhaa bora ambazo zitakidhi matakwa ya viwango vya kitaifa na kimataifa.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka wajasiriamali mkoani humo, kuzingatia kanuni zote za ubora, usalama wa chakula na mahitaji ya soko ili kuweza kuzalisha bidhaa bora ambazo zitakidhi matakwa ya viwango vya kitaifa na kimataifa.
Babu ametoa rai hiyo leo Jumatatu, Septemba 9, 2024 wakati akifungua mafunzo kwa wajasiriamali kutoka Wilaya za Mwanga, Moshi na Hai mkoani humo, yanayohusu uzingatiaji wa viwango vya ubora, usalama wa chakula na mahitaji ya soko.
Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa kuhakikisha wajasiriamali nchini wanapata maarifa ya kutosha na uwezo wa kujikinga dhidi ya changamoto zinazohusiana na viwango vya ubora na usalama wa chakula.
"Kupitia mafunzo haya mtaimarika na kuhakikisha bidhaa zenu zinaingia katika masoko ya ushindani ya ndani na nje ya nchi, na ili kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazoweza kushindana sokoni ni vizuri kuzingatia ubora wa viwango na usalama wa chakula".
Ameongeza kuwa"Serikali inayongozwa kwa umahiri mkubwa na kiongozi wetu shupavu Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wadau wetu ili kuhakikisha wajasiriamali wanapatiwa mafunzo na kuzalisha bidhaa zinazokidhi ubora wa kitaifa na kimataifa"
"Naamini kupitia mafunzo haya mtaimarika na kuhakikisha bidhaa zenu zinaingia katika masoko ya ushindani ya ndani ya nchi za nje".
Aidha mkuu huyo pia amewataka wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa wanazozalisha Mkoa wa Kilimanjaro, zinauzwa mikoa mbalimbali nchini na hata nje ya nchi.
"Hamtakiwi kuuza bidhaa zenu ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro au Moshi kama Kisiwa, mnatakiwa kutoka kwenda mikoa mbalimbali hata nje ya nchi, kwani mafunzo haya yanalenga kuwawezesha kuwa wafanyabiashara wakubwa, yaani kama sasa hivi una gari aina ya kirikuu baada ya miezi kadhaa au mwaka wakaone umenunua Canter, kama una mashine ndogo, baada ya mwaka wakuone na mashine kubwa ya kisasa"amesema Babu.
Amesema "Kumbukeni kwamba mnapaswa kuzingatia kanuni zote za ubora na usalama wa chakula na mahitaji ya soko ili kuleta bidhaa bora ambazo zitawasaidia kuongeza thamani ya uzalishaji wenu,” amesema.
Mratibu wa mradi wa Qualitan toka shirika la umoja wa mataifa la maendeleo ya viwanda (Unido) Valency Mutakyamirwa amesema lengo kubwa la mradi huo ni kuwajengea uwezo wajasiriamali na kuwawezesha kukidhi matakwa ya viwango ili kupenya kuyafikia masoko ya kikanda na kimataifa.
"Mradi huu unatekelezwa na Unido kwa kushirikiana na shirika la viwango Tanzania TBS na kufadhiliwa na umoja wa ulaya, hapa tunawaelimisha na kuwafahamisha wajasiriamali mahitaji na taratibu za kufanya ili waweze kukidhi matakwa ya masoko mbalimbali na kuwajengea ufahamu juu ya masoko yaliyopo katika kanda tofauti ambako wanaweza kupeleka bidhaa zao,” amesema
Kaimu Mkurugenzi wa mafunzo na usimamizi wa mikoa kutoka Shirika la viwanda vidogo vidogo(Sido), Stephen Bondo amesema mafunzo hayo ambayo yanatolewa kupitia mradi wa Qualitan yanalenga kuwafikia wajasiriamali 100 katika Mkoa wa Kilimanjaro na lengo ni kuwawezesha kupata ujuzi wa kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora Kitaifa na Kimataifa.
"Mafunzo ya leo yamekutanisha wajasiriamali 25 kutoka Mkoa wa Kilimanjaro ambao ni wazalishaji wa unga wa mahindi,kimsingi wanapatiwa ujuzi ili waweze kuzingatia kanuni na taratibu za kuzalisha bidhaa zao,à ziwe bora na kukidhi viwango vya ubora" mesema Bondo.
Ameongeza kuwa, "Kwa mkoa mzima watafikiwa walengwa 100 na programu hii inalenga mikoa 10 ambapo watafikiwa wajasiriamali 1,000 na tayari tumetoa mafunzo katika mikoa sita".
Said Makange mmoja wa wajasiriamali wanaopatiwa mafunzo hayo, ameomba kurahisishiwa utaratibu wa kupata viwango vya ubora (Tbs) katika bidhaa wanazo zalisha ili kuweza kuuza bidhaa zao maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.