RC Iringa awaapisha maDC walioteuliwa na Rais Samia

Muktasari:
- Walioapishwa ni Benjamin Sitta, Mkuu wa Wilaya ya Iringa na Estomin Kyando, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo. James amewaagiza viongozi hao kufanya kazi kwa bidii ili kutatua kero za wananchi na kuendeleza shughuli za maendeleo.
Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amewaapisha wakuu wa wilaya walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kuongoza wilaya za Iringa na Kilolo zilizopo mkoani humo.
Walioapishwa ni Benjamin Sitta, Mkuu wa Wilaya ya Iringa na Estomin Kyando, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo. James amewaagiza viongozi hao kufanya kazi kwa bidii ili kutatua kero za wananchi na kuendeleza shughuli za maendeleo.
James amefanya uapisho huo leo Juni 30, 2025 katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa kwa kuwaapisha viongozi hao walioteuliwa na Rais Samia Juni 23, 2025.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Kyando alikuwa Katibu Tawala katika wilaya hiyo wakati Sitta ni meya mstaafu wa halmashauri ya manispaa ya Kinondoni iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, RC James amewataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kufikia malengo chanya katika sekta mbalimbali.
Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita ina dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo viongozi wa wilaya wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutekeleza hilo.
“Kero za wananchi hazina likizo. Nendeni mkawasikilize, mshirikiane nao na muwe sehemu ya suluhisho la changamoto zao,” amesisitiza James.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa aliyepandishwa cheo kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, amewataka viongozi hao kuhakikisha wanaimarisha huduma za kijamii kama afya, elimu na miundombinu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Dorice Kalasa amewapongeza viongozi hao kwa kuteuliwa na kuwataka kutumia nafasi zao mpya kwa ufanisi mkubwa.
Kalasa ameeleza kuwa Serikali ya mkoa ipo tayari kushirikiana nao kwa karibu kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa tija na kwa manufaa ya wananchi.
Kalasa ametumia fursa hiyo kumkaribisha rasmi James katika mkoa huo, akiahidi kutoa ushirikiano wa karibu kutoka kwa watumishi wote wa sekretarieti ya mkoa.
Viongozi hao wapya wameahidi kuanza kazi mara moja na kuweka kipaumbele katika kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili kila siku.
“Naomba nimshukuru Mungu na Rais Samia, mengi umeyaongea mazuri na nilichojifunza Iringa inahitaji ushirikiano, hivyo nitajitahidi,” amesema DC Sitta.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Kyando amesema: “Nashukuru kwa nafasi hii lakini niseme kuwa nitafanya kazi na Mungu aniongoze.”
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Romanus Mihali, aliyehudhuria hafla hiyo amesema wataendelea kuwaombea viongozi ili wafanye kazi bora zaidi.
”Kiukweli leo hii tukiulizwa kuwa imekuaje viongozi hawa mpaka wakachaguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hakika jibu ni Mungu ameamua kutenda,” amesema.