Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Mtambi akemea ubadilishaji michoro ya miradi bila kibali

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bunda kilichoitishwa kujadili hoja za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke.

Muktasari:

  • Kanali Mtambi ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Juni 22, 2026, mjini Bunda wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Bunda. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia michoro na mikataba inayotolewa na Serikali huku akionya dhidi ya tabia ya kubadili michoro ya miradi kwa madai ya ufinyu wa bajeti bila kufuata taratibu zilizowekwa.

Kanali Mtambi ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Juni 22, 2026, mjini Bunda wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Agizo hilo limekuja kutokana na hoja ya CAG iliyobaini kuwa halmashauri hiyo ilifanya mabadiliko ya michoro katika baadhi ya miradi ya maendeleo bila kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-Tamisemi, kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za Serikali.

Akizungumza katika kikao hicho, Kanali Mtambi amesema Serikali huandaa michoro ya miradi kwa kuzingatia viwango maalumu vinavyolenga kuhakikisha miradi hiyo inatoa huduma zinazokusudiwa, inadumu kwa muda mrefu na kuleta thamani halisi ya fedha za umma.

Amesema mabadiliko ya michoro bila kufuata utaratibu yanaweza kusababisha utekelezaji wa miradi isiyokidhi viwango vinavyotakiwa, jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.

“Mnapoamua kufanya mabadiliko ya michoro bila kibali, mnaweza kusababisha miradi kutekelezwa chini ya kiwango. Fuateni utaratibu na tumieni michoro iliyoidhinishwa ili kuhakikisha miradi inajengwa kwa viwango stahiki,” amesema Kanali Mtambi.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bunda wakiwa katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke.

Aidha, ameagiza halmashauri hiyo kufanya marekebisho katika miradi yote iliyofanyiwa mabadiliko ya michoro na kuhakikisha inatekelezwa kwa kutumia michoro iliyoelekezwa na wizara husika, huku gharama za marekebisho hayo zikibebwa na halmashauri.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda pamoja na menejimenti yake, kuimarisha usimamizi wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalumu ili kuhakikisha walengwa wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Agizo hilo limetokana na hoja ya CAG iliyoonyesha kuwa utoaji wa mikopo hiyo haukuzingatia mgawanyo wa asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu, kama inavyoelekezwa na mwongozo wa Serikali.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sehemu ya fedha zilizotengwa kwa vijana na watu wenye ulemavu zilihamishiwa kwenye kundi la wanawake kabla ya kupatikana kibali cha kufanya hivyo.

Kanali Mtambi amesema hatua hiyo inaashiria kutokuzingatiwa kwa taratibu za utoaji wa mikopo hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuwafikia walengwa badala ya kusubiri waombe mikopo kwa hiari yao.

“Kuna kitu hakiko sawa hapa. Maofisa wanaosimamia mikopo wanapaswa kuwafikia walengwa, kuwapatia elimu na kuwahamasisha kutumia fursa hizi. Fursa zipo, lakini wengi wanakosa taarifa na elimu ya kutosha,” amesema.

Akijibu hoja kuhusu mabadiliko ya michoro, Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Tiopatila Chaula amesema uamuzi huo ulifanyika katika mradi wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Kabasa kutokana na fedha zilizotolewa kutotosheleza gharama zilizokuwa zimeainishwa kwenye mchoro wa awali.

Amesema mradi huo ulipokea Sh130 milioni wakati makadirio ya utekelezaji kwa mujibu wa mchoro yalikuwa zaidi ya Sh167.6 milioni.

“Kutokana na tofauti hiyo ya fedha, tulifanya marekebisho katika baadhi ya vipengele vya ujenzi. Badala ya kuweka vigae tuliweka sakafu ya kawaida, na badala ya mabati ya rangi tulitumia mabati meupe ili fedha zilizopatikana ziweze kutosha kukamilisha mradi,” amesema Chaula.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Ladislaus Magaso amesema fedha za mikopo zilihamishwa kwenda kwa wanawake kutokana na idadi kubwa ya maombi kutoka kundi hilo ikilinganishwa na vijana na watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, viongozi wa Serikali wameitaka halmashauri kuhakikisha taratibu zote za utoaji wa mikopo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinafuatwa ili kuondoa hoja zinazojitokeza katika ukaguzi wa hesabu za Serikali na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma.