RC Shinyanga azuia tani 400 za dengu kusafirishwa

RC Shinyanga azuia tani 400 za dengu kusafirishwa

Muktasari:

  • Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk Phillemon Sengati amezuia zaidi ya tani 400 za dengu zinazodaiwa kununuliwa kutoka kwa wakulima kwa njia ya ulanguzi zisisafirishwe nje ya mkoa huo.

Mwanza. Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk Phillemon Sengati amezuia zaidi ya tani 400 za dengu zinazodaiwa kununuliwa kutoka kwa wakulima kwa njia ya ulanguzi zisisafirishwe nje ya mkoa huo.

Dk Sengati ameagiza shehena hiyo ambayo ilikuwa imepakiwa kwenye malori tayari kwa kusafirishwa, ishushwe na kuhifadhiwa kwenye magala ya Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos) na Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (Shirecu) kusubiri mnada.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Agosti 24, Dk Sengati amesema uamuzi huo siyo tu unalinda maslahi ya wakulima watakaopata bei nzuri na yenye ushindani, bali utawezesha halmashauri na Amcos kupata mamilioni ya fedha kupitia ushuru.

"Hatujataifisha mazao hayo kama baadhi ya watu wanavyoeneza na kupotosha kupitia njia ya mitandao ya kijamii; Serikali ya mkoa imeagiza mazao yote yahifadhiwe kwenye maghala ya ushirika na yauzwe kwa njia ya mnada kama ilivyo maelekezo ya Serikali ya mwaka 2019 yaliyosisitizwa tena mwaka 2020," amesema Dk Sengati

Ameongeza; "Mimi sina maelekezo au mwongozo mwingine kuhusu ununuzi wa mazao ya dengu, ufuta, choroko na mbaazi zaidi ya njia ya mnada kupitia Amcos. Hilo ndilo nalisimamia,"

Amesema mazao yote yanayohifadhiwa katika maghala ya Amcos na Shirecu yataanza kuuzwa kesho Jumatano Agosti 25 kwa njia ya mnada kupitia Soko la mnada kwa njia ya mtandao.

"Kupitia soko hilo, wanunuzi wakubwa wa dengu kutoka ndani na nje ya nchi watashindana kwa bei na hivyo kuwanufaisha wakulima," amesema Dk Sengati

Maelezo ya Mkuu huyo wa mkoa yamekuja baada ya kusambazwa mitandaoni kwa kipande cha video kikionyesha shehena hiyo inavyoshushwa na taarifa zikizunguka kuwa Serikali mkoani humo imezuia shehena ya mazao yaliyopakiwa kwenye malori kusafirishwa nje ya mkoa huo.

Huku akisita kutaja majina, Mkuu huyo wa mkoa amedai uamuzi wake umesababisha mgongano kati yake na baadhi ya viongozi wakiwemo wabunge ambao wengine ni wafanyabiashara wa mazao hayo wanaojaribu kushinikiza mazao hayo yaruhusiwe kusafirishwa bila kufuata utaratibu stakabadhi ghalani na mnada.


"Kupitia mnada wakulima wanapata bei nzuri kuanzia zaidi ya Sh1, 100 kwa kilo kukinganisha na Sh700 hadi Sh900 wanayolipwa na walanguzi," amesema


Kwa mujibu wa Dk Sengati, mkoa wa Shinyanga unatarajiwa kuvuna zaidi kilo milioni 7 za dengu ambazo zitaingizia halmashauri za mkoa huo mapato ya zaidi ya Sh500 milioni iwapo zitauzwa kupitia stakabadhi ghalani na njia ya minada.

"Amcos zetu zitaingiza zaidi ya Sh300 milioni kupitia ushuru na tozo mbalimbali za kusimamia mauzo na ununuzi wa mazao yanayouzwa kwa njia ya stakabadhi ghalani. Fedha zote hizo zitapotea tukiruhusu uuzaji na ununuzi holela kwa sababu baadhi ya wanunuzi siyo wakweli kwenye taarifa zao wanazowasilisha kwenye mamlaka," amesema Dk Sengati