Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rehema: Nilitamani niwe mwalimu, sijutii kuwa mamalishe

Safari yake kutoka kijijini Mashewa mkoani Tanga kuja jijini Dar es Salaam ililenga kusaka elimu, siku zote alikuwa na ndoto za kusoma na kupata taaluma itakayomwezesha kuendesha maisha yake na ya familia.

Wakati anasoma shule ya msingi ndoto yake ilikuwa aje kuwa mwalimu akiamini ndiyo kazi aliyoipenda na anaendana nayo.

Si kuipenda fani hiyo tu, alitamani azungumziwe kati ya watu waliofanikiwa kupitia elimu na ualimu ndiyo ilikuwa chaguo lake la kwanza kabla ya maisha kumpeleka upande mwingine.

Huyu ni Rehema Ally (35), mama wa mtoto mmoja ambaye kwa sasa anaendesha maisha yake kwa biashara ya mamalishe aliyoifanya kwa takribani miaka saba kuanzia kuajiriwa kwa ujira mdogo hadi kujiajiri.

Wakati dunia ikiwa katika juma la kuadhimisha siku ya wanawake Machi 8, mama huyu ni miongoni mwa wanawake wapambanaji ambao kamwe hawakubali kukata tamaa, licha ya changamoto wanazopitia.

Ndoto yake ya ualimu iliyeyuka akiwa darasa la nne baada ya kupata ujauzito, hivyo kulazimika kukatisha masomo na kuanza malezi ya mimba na baadaye mtoto akiwa kwao Tanga.

Miaka miwili ya kulea ujauzito na mtoto ilivuruga maisha ya Rehema, hivyo akajikuta anashawishika kurudi jijini Dar es Salaam kujitafutia kipato, akifahamu fika hana taaluma yoyote lakini akapiga moyo konde na kufanya uamuzi.

“Maisha yalikuwa magumu, ukumbuke mimi nilikuwa mdogo halafu nikapata mtoto, sina chanzo chochote cha mapato kuniwezesha kumudu gharama za maisha. Baada ya kuwaza na kuwazua nikaona ni heri nirudi mjini kuja kutafuta maisha.

“Kwa kuwa sikuwa na elimu hakuna kazi niliyofikiria zaidi ya mamalishe, nilifanikiwa kupata kazi Magomeni ambako nilikuwa nalipwa Sh2,000 kwa siku nikisaidia shughuli zote za mgahawani,” anasema Rehema.

Licha ya kiwango hicho kuwa kidogo, hakuwa na budi ya kukubaliana na hilo na kuanza kazi kwenye banda la mamalishe akiwa mhudumu. Hata hivyo, umahiri wake katika upishi ukamfanya aaminike jikoni.

Haikumchukua muda mrefu kabla ya kupata kazi eneo lingine ambalo alikabidhiwa kuendesha mgahawa akiwa mpishi mkuu kwa ujira wa Sh5,000 kwa siku.

“Hiki kibarua cha pili nilipata pale maeneo ya Sinza, nilikabidhiwa kuuendesha mgahawa. Kwa kuwa chakula nilikuwa napika na kupakua mimi nilikuwa nahakikisha naongeza idadi ya sahani ili niweze kuondoka na chochote kitu,” anasema.

“Nilikuwa naongeza idadi ya sahani, kwa mfano natakiwa nitoe 20, nilikuwa nahakikisha zinapatikana 25, kwa njia hii nilijiwekea lengo la kuondoka na kiasi fulani na kila siku ilikuwa lazima niondoke na Sh15,000,” anasema.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha ya kujitegemea akiwa Dar es Salaam, alidumu katika ajira hiyo kwa miaka miwili kabla ya kukusanya kiasi cha fedha cha kutosha kumwezesha kufungua biashara yake na kuendesha maisha.

Kwa akiba aliyoweka aliweza kupanga chumba na kubakiwa na kiasi cha fedha alichokitumia kama mtaji na kodi ya kulipia banda la biashara alilopata. Rasmi akaingia kwenye kazi ya mamalishe. Kutokana na uzoefu aliopata kwenye biashara hiyo katika maeneo aliyowahi kuajiriwa haikumuwia vigumu kuanzisha yake na kuendelea kusimama kwa takribani miaka mitano mfululizo, licha ya changamoto za hapa na pale.

“Kwa kweli mamalishe tunakabiliwa na changamoto nyingi, ukiamua kuzikumbatia na kuruhusu zikuumize kichwa huwezi kuendelea, lakini ukizichukulia ni sehemu ya kazi utayaona matunda ya biashara hii.


Gharama bei za bidhaa

Kupanda bei za vyakula ndilo tatizo linalomsumbua zaidi Rehema kwa sasa, kwa kuwa hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kuyumbisha biashara.

Anasema katika kipindi chote tangu aingie kwenye biashara hiyo amekuwa akikutana na adha ya kupanda kwa bei za bidhaa anazotumia, lakini ongezeko hilo haliendi sambamba na kuwapandishia bei wateja wake.

“Mteja huwezi kumwambia unapandisha sahani ya wali kwa sababu mchele umepanda bei au nyama imepanda bei, ukifanya hivyo utawakimbiza, sasa ili waendelee kuwepo inabidi wakati mwingine uumie wewe mambo yaende.

“Sasa hivi kuna changamoto ya kupanda kwa bei ya sukari, huwezi kumwambia mtu chai imepanda bei akakuelewa, ili kuondoa migongano nalazimika kuacha kupika chai, nitapika supu na chakula cha mchana ila kwa ukweli wafanyabiashara wadogo tunaumia zaidi katika hili,” anasema.

Rehema hakubaliani na watu wanaoidharau kazi hiyo kwa kuwa imebadili kwa kiasi kikubwa maisha yake, kutoka kwenye utegemezi hadi yeye kutegemewa, akiwahudumia mama na wadogo zake.

Anasema: “Huwa nawashangaa zaidi wanawake ambao hawajishughulishi na kitu chochote, maisha ya sasa mwanamke huwezi kujivunia kuwa tegemezi, ukae nyumbani usubiri kuletewa. Kitu ninachoweza kuwaeleza wanawake wenzangu hakuna hela tamu kama ya kuitafuta mwenyewe.

“Ule uchungu unakuwa nao kwenye utafutaji ndiyo utakuwa nao hata kwenye matumizi, kama unatafuta mwenyewe unakuwa na nidhamu ya hali ya juu na uhuru wa fedha yako kwenye matumizi, si kusubiri kuletewa, najivunia kuwa miongoni mwa wanawake wanaojitafutia,” anasema.

Si kuendesha maisha tu na kupata mkate wa kila siku, biashara ya mamalishe imemwezesha pia kutimiza lengo la kumjengea nyumba mama yake aliye kijijini. Anasema yupo katika mchakato wa kujenga nyumba jijini Dar es Salaam.

Anasema wakati anakuja Dar lengo lake lilikuwa kutafuta maisha, lakini kwa jitihada anazoendelea kuziweka ana uhakika maisha yake ya kudumu yatakuwa kwenye jiji hilo la kibiashara kwa kuwa tayari ameshapata ardhi.

“Huwa siumizwi kichwa na wanaonichukulia poa, naheshimu kazi yangu kwa kuwa ni kazi kama ilivyo nyingine. Kupitia kazi hii nimeweza kuwa na lengo la siku moja niondoke kwenye nyumba ya kupanga, nimeshapata eneo, naamini ipo siku nitajenga,” anasema.


Wito kwa wasichana, wazazi

Rehema anakiri kupata ujauzito katika umri mdogo kulimfanya apoteze mwelekeo wa maisha, hivyo hatamani kuona msichana yeyote akiangukia kwenye changamoto hiyo.

Katika hilo msisitizo wake kwa watoto wa kike ni kuweka mkazo kwenye elimu ili iwe rahisi kutimiza ndoto zao kwa kuwa elimu ndiyo msingi wa kila kitu.
“Natamani watoto wa kike waone umuhimu wa elimu, wasishawishike kuingia kwenye mambo yasiyofaa kwa kuwa msingi wa maisha ni elimu, hata kama unafanya biashara ndogondogo ukiwa na elimu inakusaidia.

“Kama umepata nafasi ya kusoma basi soma kwa juhudi na maarifa usichanganye na vitu vingine, niwasihi pia wazazi wawe kichocheo cha kuhamasisha watoto wa kike wasome. Mzazi wajibika kumwekea mwanao mazingira wezeshi ili asishawishike na mambo mengine,” anasema.


Fursa sawa kwa wanawake

Moja ya mikakati kamambe inayotekelezwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni usawa na uwezeshaji wa wanawake na vijana nchini, kunufaika na fursa mbalimbali za uwezeshwaji kiuchumi.

Pia, uwezeshaji huo umegusa maeneo mengine, ikiwemo mazingira bora ya kufanyia shughuli, kuondolewa kwa baadhi ya kodi na tozo na miundombinu, yakiwemo majiko ya gesi ikiwa ni mkakati wa kuondokana na matumizi ya kuni yanayosababisha madhara makubwa kiafya.

Hili limefanywa zaidi kwa mamalishe kwenye mikoa mbalimbali nchini, Rais Samia alitoa majiko ya gesi yaliyofikishwa kwa wahusika kupitia wabunge na madiwani.

Hata hivyo, si wanawake wote wanaotambua au kufikia fursa hizo kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi na wengine kukatishwa tamaa pindi anapojaribu kupata taarifa au kushindwa baadhi ya masharti yanayowekwa.

Kwa mfano, Rehema anasema anafahamu fursa mbalimbali zilizoibuliwa na Serikali ya Rais Samia, lakini bado hajawa miongoni mwa waliojaribu kutokana na masharti kuwataka kuwa kwenye kikundi.

“Natambua kuna fursa nyingi za mikopo kwa wajasiriamali wanawake, lakini ipo ile ya halmashauri ya asilimia 10 ila inanihitaji nijiunge kwenye kikundi ndipo nipate. Sasa mnaweza kujiunga kwenye kikundi mkapewa fedha, lakini mmoja wenu akashindwa kurejea na mliobaki mnaweza kujikuta mnabeba jukumu,” anasema.

“Kama itatokea mikopo hiyo kutolewa kwa mtu mmoja mmoja basi nitaenda kuchukua, hii ya kikundi inanipa hofu kwa sababu sifahamu wenzangu watakuwa tayari kurejesha ili wengine wakopeshwe,” anasema Rehema.

Tayari Serikali imezindua Baraza la Taifa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi na kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuendelea kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume kushiriki nafasi za uongozi na fursa za mikopo ya biashara ili kujiendeleza.

Mbali na hilo, Baraza hilo limehimiza wanawake kushiriki kwenye ngazi za maamuzi kwenye jamii na kuwa sehemu ya maamuzi kwa ustawi wa jamii na Taifa.
Akizindua baraza hilo mwaka jana, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema pamoja na mambo mengine, Baraza hilo litakuwa njia ya kumkwamua mwanamke kiuchumi.

“Jukwaa hili lihakikishe wanawake wote wanaona na kupata fursa ya kujiunga na majukwaa yaliyopo kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa, kata, wilaya hadi Taifa ili yawawezeshe kupata sehemu ya kujadili mambo yao kuhusu ujasiriamali na biashara kwa jumla.

“Nazitaka Halmashauri za Wilaya/ Manispaa na Majiji kuendelea kutenga fedha za ndani ili kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo kujiendeleza kiuchumi,” alisema.