Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ridhiwani: Msajili wa Hazina ameokoa mashirika ya umma

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina imeimarisha kifedha mashirika ya umma yaliyokuwa na hasara na mitaji hasi, sasa yakitoa gawio na kuepuka ruzuku ya Serikali. Mashirika kama Osha, Stamico, Tanesco na TPDC yameonyesha ufanisi mkubwa.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina imewezesha kuimarika kifedha kwa mashirika ya umma yaliyokuwa na mitaji hasi na yaliyokuwa yanapata hasara mfululizo.

Kikwete amesema hayo leo, Julai 5, 2025 alipotembelea na kukagua Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DiTF) maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Kikwete ameishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuwezesha mashirika ya umma kuongeza ufanisi wao.

“Kupitia ofisi hii, mashirika ya umma yaliyokuwa na mitaji hasi na yaliyokuwa yanapata hasara mfululizo sasa yameweza kuondokana na utegemezi wa ruzuku ya Serikali na kufanikiwa kutoa gawio,” amesema Kikwete.

Baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) ambapo mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali ulikuwa Sh10.5 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25.

Pia, katika orodha ya mashirika ambayo kwa sasa yanajiendesha kwa ufanisi ni Shirika la Taifa la Madini (Stamico), Shirika la Umeme (Tanesco) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Ili kuendeleza mageuzi hayo, amesema Serikali itaendelea kuiunga mkono Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kuhakikisha safari ya mageuzi inafanikiwa.

“Endeleeni kufanya kazi kwa bidii na pale ambapo kuna mambo mnataka yabadilike katika taasisi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hesabuni mmepata ushirikiano kutoka kwetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri amesema kumekuwa na ongezeko la ufanisi kwenye baadhi ya mashirika kutokana na mageuzi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika mashirika ya umma.

“Ufanisi umeimarika kwa kiasi kikubwa, mfano mzuri tunauona kwenye Mamlaka ya Bandari,” amesema Kosuri.

Kwa mwaka wa fedha uliopita, pamoja na kuongeza mchango kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kutoka Sh155.7 bilioni mwaka 2023/24 hadi Sh181 bilioni mwaka 2024/25, matumizi ya kawaida kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa bandari pia yamepungua kwa kiasi cha Sh505.59 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 46.

“Tunaishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya uongozi imara wa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kwa ufanisi huu,” amesema Kosuri.