Ripoti ajali ya Precision yapigilia msumari uzembe

Dar es Salaam. Wakati kamati iliyoundwa kuchunguza chanzo cha ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air ikitoa ripoti ya awali inayoashiria uzembe katika huduma za uokoaji, wadau wa usafiri wa anga wamependekeza hatua za haraka zichukuliwe kuepuka majanga siku zijazo.

Ripoti hiyo ya awali iliyosambaa juzi na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje, juzi imechambua mambo mbalimbali ya kitaalamu yaliyotokea wakati wa ajali hiyo na kuwa uchunguzi zaidi wa chanzo cha tukio hilo unaendelea.

Baada ya ajali hiyo iliyotokea Jumapili ya Novemba 6, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 19 na 24 kuokolewa, timu tatu zilianza uchunguzi ambazo ni kitengo maalumu cha uchunguzi cha ajali za anga, kampuni iliyotengeneza ndege na iliyotengeneza injini.

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo ya awali ya kitengo cha uchunguzi cha ajali za anga katika Wizara wa Ujenzi na Uchukuzi, imeweka wazi kuwa askari wanamaji walipewa taarifa dakika 15 baada ya ajali na walishindwa kufika eneo la tukio mapema kwa kuwa boti ya uokozi ilikuwa mbali kwenye doria.

Mbali na boti hiyo, askari hao walikwama kuzamia na kufika eneo hilo, kwa kilichobainishwa na ripoti hiyo yenye kurasa saba, kuwa mitungi ya oksijeni waliyokuwa nayo haikuwa na gesi hiyo.

Mabadiliko ghafla ya hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Mkoa wa Kagera iliyosababisha mvua, wingu zito na radi ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kutokea siku ya tukio kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo Mwananchi limeiona.

“Hali ya hewa ilikuwa nzuri hadi saa 2:20 asubuhi, ilibadilika ghafla mvua ikaanza kunyesha na radi, mawingu mazito na upepo mkali,” imeeleza ripoti hiyo.

Hata hivyo, ripoti hiyo imependekeza kwa Serikali kuongeza uwezo wa vitengo vya uokoaji katika viwanja vya ndege na huduma za zimamoto na uokozi majini ili kutekeleza operesheni za utafutaji na uokoaji wakati wa janga.

Ilipendekeza kutengenezwa utaratibu mzuri wa utafutaji na uokoaji katika matukio na uwepo muundo imara ulioratibiwa katika huduma za uokoaji na utafutaji katika usafiri wa majini na anga.

Kwa waongozaji ndege wanaofanya safari za kwenda Bukoba, ripoti ilipendekeza wafanye tathmini ya mara kwa mara kujua hatari ya usalama wa shughuli zao katika eneo husika.

Sehemu kubwa ya mapendekezo hayo yanashabihiana na yale yaliyotolewa na wadau wa usafiri wa anga, wataalamu wa majanga na Baraza la Mawaziri lililoketi kwa dharura Novemba 14 mwaka huu kujadili suala hilo.

Baada ya kikao cha mawaziri chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema kimewaagiza wataalamu wa ndani kushirikiana na wa nje kufanya uchunguzi wa ajali hiyo ili kupata chanzo cha ajali na kutoa mapendekezo.

Kwa mujibu wa Msigwa, Baraza hilo lilielekeza vitengo vinavyohusika na kukabiliana na majanga kuimarishwa ili kuiwezesha nchi kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga.

Baraza hilo liliketi siku nane baada ya ajali huku wadau na wataalamu mbalimbali wakiwa wametoa maoni yanayoonyesha kuwa kilichotokea kilitokana na uzembe katika uokoaji.


Hatua za haraka

Saa chache baada ya ripoti ya awali kusambaa, Lathifa Sykes, katibu mtendaji wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (Taoa) alizungumza na Mwananchi akitaka hatua zichukuliwe sasa kwa kuwa ajali hii si ya kwanza kutokea.

“Tunapaswa kuchukua hatua, hii si mara ya kwanza ajali kama hiyo kutokea,” alisema, akikumbushia kilichotokea kutokana na meli ya Mv Bukoba kuzama katika Ziwa Victoria mwaka 1996 na kusababisha vifo zaidi ya 800 kuwa kitumike kama funzo.

Hata hivyo, alisema Serikali haiwezi kufanya hili peke yake, bali ni vema sekta binafsi ikashirikishwa.

Alishauri sekta hiyo ikae na Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na kujadili mbinu za pamoja za kukabiliana na janga kama hilo.

Alichokipendekeza Lathifa kinaungwa mkono na mtaalamu katika sekta ya usafiri wa anga, Juma Fimbo aliyefananisha kilichotokea katika ajali ya ndege ya Precision Air na tukio la Mv Bukoba.

Alisema mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyoundwa kuchunguza ajali hiyo ya miaka 26 iliyopita, yanafanana na mapendekezo na kamati ya Precision Air katika ripoti hiyo ya awali.

“Tumechelewa sana, tulipaswa kuchukua hatua tangu jana. Lakini angalau tuchukue hatua sasa na si kesho,” alisema Fimbo.

Hata hivyo, Fimbo alisema ni vigumu kwa Tanzania pekee kuwa na timu imara ya utafutaji na uokozi, kwa kuwa unahitajika uwekezaji mkubwa wa rasilimali fedha kwa ajili ya vifaa, mafunzo na majaribio.

Alipendekeza umuhimu wa mataifa yote yanayozunguka Ziwa Victoria kushirikiana katika kuunda programu ya dharura ya kukabiliana na majanga hayo.

“Tunapaswa kuunganisha nguvu ili kukusanya rasilimali, iwapo kila nchi itafanya peke yake juhudi zetu hazitatosheleza,” alieleza mtaalamu huyo.

Hata mtazamo wa Innocent Kyara, katibu mtendaji wa Baraza la Watumiaji wa huduma za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA-CCC) hauna tofauti na wenzake, akisema umefika wakati wa Serikali kufanyia kazi mapendekezo ya ripoti za uchunguzi wa ajali.

“Juhudi zetu zinapaswa kuwa kwenye kuchunguza na kudhibiti majanga, kuliko kujiandaa kuyakabili,” alisema.


Nani alifungua mlango?

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uchunguzi wa mabaki umeonyesha kuwa ilikuwa vigumu kufungua mlango wa ndege wa nyuma kwa kuwa tayari ulikuwa umezama ndani ya maji.

“Mhudumu mmoja ndiye aliyefungua mlango wa kushoto wa abiria, alisaidiwa na abiria mmoja kuusukuma. Baadhi ya manusura, akiwemo mtoto mwenye miezi 18 na mama yake waliokolewa kwa njia hiyo,” inaeleza ripoti hiyo.

“Wavuvi walikuja dakika tano baadaye na waliwapakia manusura katika boti yao, kwa hiyo abiria 24 wakiwemo wahudumu wawili walipona.

“Ndege hiyo ilianguka majini umbali wa mita 500 kutoka njia ya kurukia ndege. Kina cha maji katika eneo hilo kilikuwa mita 5.4,” alisema.

Kabla ya ndege hiyo kuanguka majini na kuharibika sehemu yake ya mbele na uharibifu zaidi kutokea wakati wa kuivuta, rubani aliizungusha katika uwanja wa ndege wa Bukoba kwa takriban dakika 20, ripoti hiyo imeeleza.

Kulingana na ripoti hiyo, haukuwa uamuzi wake rubani kuiangusha ndege hiyo ziwani, badala yake alitaka kuipeleka Mwanza kwa ajili ya kutua kwa dharura na kwamba abiria walitaarifiwa hivyo na wahudumu.

Wengi kati ya abiria waliofariki, vifo vyao vilisababishwa na maji yaliyoingia katika ndege hiyo.