RIPOTI: Wengi wanaochepuka hawatumii kinga

Muktasari:

  • Ripoti hiyo ya Utafiti wa Afya, Malaria na Viashiria (Tanzania DHS-MIS 2022) iliyotolewa na wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonyesha kuwepo kwa idadi kubwa ya ufanyaji wa ngono zembe kwa ‘michepuko’ hali inayoweza kusababisha ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU).

Dar es Salaam. Wakati takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) zikionyesha maambukizi ya ugonjwa huo yameshuka kwa asilimia 47, ripoti mpya ya Wizara ya Afya imeonyesha viashiria vya uwezekano wa kuongezeka kwa virusi kutoka kwa wasiokuwa wanandoa wala wachumba (michepuko).

Ripoti hiyo ya Utafiti wa Afya, Malaria na Viashiria (Tanzania DHS-MIS 2022) iliyotolewa na wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonyesha kuwepo kwa idadi kubwa ya ufanyaji wa ngono zembe kwa ‘michepuko’ hali inayoweza kusababisha ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU).

“Asilimia 22 tu ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 waliohojiwa walifanya ngono kwa kutumia kondomu kwa ‘michepuko’ yao huku wanaume wa umri huo asilimia 43 pekee ndio walitumia kondomu walivyoshiriki tendo hilo na ‘michepuko’ yao,” ripoti inaeleza.

Takwimu hizo zinamaanisha wanawake wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi na magonjwa ya zinaa kutokana na kushiriki ngono kwa kiasi kikubwa na wanaume wasio waume wao bila kinga.

Asilimia hiyo ni sawa na mwanamke mmoja kati ya watano wanaoshiriki ngono na ‘michepuko’ hawatumii kondomu. Pia, wanaume wawili kati ya watano wanaoshiriki ngono na wanawake ‘michepuko’ hawatumii kondomu.

Vilevile, katika kuonyesha kuwa hatari ya kuenea na kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi inazidi kuwa kubwa, ripoti hiyo imeonyesha wastani wa kila mwanamume mmoja amewahi kushiriki ngono na wanawake 8.3

Kwa upande wa wanawake, ripoti inaonyesha wastani wa kila mwanamke amewahi kushiriki ngono na wanaume 3.2 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49.

Hata hivyo, ripoti hiyo imeitaja mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Dodoma kuongoza kuwa na watu wanye wapenzi zaidi ya wawili.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa juzi Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu inaeleza takwimu zinazohusu maambukizi ya Ukimwi zitasaidia kwenye kudhibiti ugonjwa huo.

“Taarifa kuhusu tabia ya kujamiiana ni muhimu katika kutunga na kufuatilia mipango ya kudhibiti kuenea kwa Virusi vya Ukimwi (VVU),”inaeleza ripoti hiyo.

Zainab Abdallah, daktari katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa MKoa wa Lindi alisema tabia za kuwa na wapenzi wengi na kushiriki ngono bila kondomu inaweza kusababisha VVU na magonjwa ya zinaa. “Kuna uwezekano mkubwa sana wa kuongeza maambukizi ya VVU kwenye jamii, kwa sababu kama ripoti inaonyesha ‘michepuko’ wengi ndo hawatumii kondomu unaweza kuona hatari iliyopo hapo,” alisema Zainab.

“Pia, mtu anakuwa katika hatari zaidi ya kupata magonjwa ya ngono kama vile kaswende na kisonono hali kadhalika UTI (njia ya mkojo).”

Magreth Samwel (22), mkazi wa Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam alisema chanzo cha watu wengi kuwa na wapenzi wa ziada ni tamaa na kulipiza kisasi.

“Kwa upande wa wanawake wengi wanatafuta wanaume wengine kwasababu ya kukidhi mahitaji yao ya kifedha na kimwili, labda haridhishwi na aliye naye lakini kwa wanaume naona ni tamaa za kimwili na kulipiza kisasi,”alisema Magreth.

Alisema watu wengi kwa sasa hawatumii kondomu kwa kisingizio kuwa watapunguza ladha ya mapenzi jambo alilolikanusha na kushauri elimu zaidi ya Ukimwi itolewe kwa vijana.

Utafiti wa mambo ya kijamii uliofanywa na Dk Christin Munsch wa Chuo Kikuu cha Cornell Marekani ulioitwa ‘Hali ya Ndoa na Jinsia’ ulionyesha sababu kubwa inayosababisha wenza kusalitiana ndani ya ndoa ni kutoridhishwa na hali duni ya maisha.

“Wanaume na wanawake wengi wanasalitiana kwenye mahusiano yao kwa sababu hawajaridhika na wapenzi wao huku hali duni ya kifedha ikiwa na mchango mkubwa kwenye hilo,”ripoti ya utafiti huo inaeleza.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) , Sheikh Khamis Mataka alisema kitendo cha kuzini na watu tofauti na mwenza wako inasababishwa na ukosefu wa maadili na hofu ya Mungu.

“Sababu kubwa inayosababisha hiyo zinaa ni ukosefu wa maadili na kupungua kwa hofu ya Mungu baina ya watu na nafsi zao kwenye jamii,”alisema Sheikh Mataka.

“Siku zote mtu mwenye hofu ya Mungu hawezi kufanya maovu hata sirini na nafsi itakayofanya hivyo kwa mujibu wa dini yetu ya Kiislamu ni sawa na ina nguvu ya mashetani 70.”

Sheikh Mataka alishauri njia ya kumaliza matatizo haya akisema,

“watu wamrudie Mungu kwa kutenda mema na kufanya ibada kama inavyoelekezwa.”

Ripoti ya Tacaids ya mwaka 2017 ilionyesha Watanzania milioni 1.4 wana maambukizi ya VVU huku maambukizi mapya yakiwa 72,000.