Ripoti ya pili ajali ya Precision yatoka, yaonyesha mambo nane

Muktasari:

  • Ripoti ya pili ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precison Air iliyotokea Novemba 6 mwaka 2022 na kusababisha vifo vya watu 19, majeruhgi 24 imetoka na kubainisha mambo nane ikiwemo marubani kutotilia maanani ishara za tahadhari zilizotolewa.

Dar es Salaam. Ripoti ya pili ya ajali ya Ndege ya Precision Air imetoka na kubainisha mambo nane yaliyochangia ndege hiyo kuanguka katika Ziwa Victoria, Bukoba, Mkoa wa Kagera.

Ndege hiyo ya Precision Air iliyotoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ilitokea Novemba 6, 2022 ambapo ilikuwa na watu 43 kati yao, 39 walikuwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili. Huku watu 19 walifariki dunia na 24 kuokolewa.

Hata hivyo, ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air, ilitoka Novemba 23 mwaka 2022, ikibainisha udhaifu katika uokozi kwa kile alichofafanua Jeshi la Polisi Kitengo cha Wanamaji kilipewa taarifa dakika 15 baada ya tukio lakini hakikufika kwa wakati.

Lakini ripoti iliyotolewa leo Jumatano Machi 22, 2023 imebainisha mambo nane ambayo ni marubani wa ndege hawakuwa na tatizo la kiafya, ndege ilikuwa imeandikishwa kihalali, hali ya hewa ya katika uwanja wa Bukoba haikuwa nzuri, hali mbaya ya hewa iliathiri marubani kutekeleza jukumu lao.

Mengine ni marubani hawakutilia maanani ishara za tahadhari zilizotolewa, ndege iligonga kwanza bawa lake la kushoto wakati ikianguka, pia ilianguka kwa kasi na kugonga sehemu ya mbele kwenye kina cha maji ya ziwa Victoria na vifaa vyote vya kuongozea ndege vilikuwa vinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya rubani.

Akizungumza na Azam TV, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege, Redemptus Bugumola amesema ripoti ya pili ina tofauti na ile ya kwanza.

Amesema ripoti ya kwanza watalaamu walikwenda eneo la tukio na kufanya tathimini ya ndege ilivyoaharibika na kuhoji wananchi.

 “Lakini hii ya pili tulikwenda mbali zaidi kama unavyojua kuna vinasa sauti ambavyo vinakuwa katika ndege. Kuna kimoja kina nasa sauti ya mawasiliano ya rubani na rubani mwenzake au matangazo yaliyokuwa yakitolewa kwa abiria,” amesema Bugumola.