Rita: Ndoa ya aina hii haitambuliki kisheria

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), cheti cha ndoa cha dini hakitoshi kukutambulisha kama mke na mume mnapofika kwenye masuala ya kisheria.
Dar es Salaam. Licha ya kufunga ndoa ya dini miaka 10 iliyopita, Jane Elias alijikuta katika sintofahamu baada ya kuambiwa ndoa yake haitambuliki kisheria.
Jane ni miongoni mwa wanandoa wengi wanaofunga ndoa katika nyumba za ibada, lakini wengi wao wanapofika kwenye sheria, hujikuta ndoa zao hazitambuliki kutokana na sababu mbalimbali.
Jane anasema alifunga ndoa ya kanisani na kupewa vyeti vya ndoa.
"Kilichonishangaza, mume wangu ambaye ni mtumishi wa Serikali, kila alipoomba likizo hakupata stahiki za mke.
"Tuliamua kufuatilia Novemba, 2024 tukaambiwa vyeti vyetu vya ndoa havitambuliki kiserikali kwa kuwa ndoa yetu haijasajiliwa, hivi sasa tupo kwenye mchakato wa kuisajili," anasema.
Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), cheti cha ndoa cha dini hakitoshi kukutambulisha kama mke na mume mnapofika kwenye masuala ya kisheria.
Rita inafafanua kwamba ili ndoa yako itambulike kisheria, lazima isajiliwe na wakala huo na kupewa cheti cha ndoa cha Serikali.
"Unaweza kuwa na cheti cha ndoa cha kanisani au msikitini na bado ndoa yako isiwe inatambulika kisheria," anasisitiza Joseph Kimaro, meneja masoko na mawasiliano wa Rita.
Sintofahamu kama hiyo imewahi kumkuta pia Mariamu Juma, aliyefunga ndoa ya Kiislamu na ile ya Serikali kwa nyakati tofauti.
"Wazazi wa mume wangu walikuwa hawanitaki, hivyo tulifunga ndoa hii kwa siri. tulikwenda Bomani, palepale tukapata mashahidi tukafungishwa ndoa, bila familia zetu kufahamu, ilikuja kuleta shida, ingawa miaka mitatu baada ya ndoa hiyo tukafunga iliyosimamiwa na Sheikh mwenye vyeti vya Rita kutoka Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata)," anasema.
Viongozi wa dini wafafanua
Suala hilo limewaibua viongozi wa dini, wakiwa na mitazamo tofauti kulingana na dini zao.
Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo anasema aliyepewa mamlaka ya kufungisha ndoa kwa dini ya Kiislamu ni walii.
"Huyu anaweza kuwa baba, kaka au baba mdogo, sisi tuko tofauti kidogo, hata kama hakuna shehe, lakini walii akitaka kufungisha ndoa ya binti yake, kwa misingi ya Kiislamu hakuna pingamizi linalomzuia kumuozesha.
Anasema japo kuna mashehe ambao ni maalumu kwa kusimamia ufungishaji ndoa ambao wanafahamika, kama ni kadhi wa kufungisha mwenye leseni za Rita na utambulisho wa Bakwata, lakini asipokuwepo, hata shehe wa kawaida anaweza kusimamia na ndoa hiyo ikawa sawa.
"Wanandoa hao wakitaka kuisajili ndoa yao lazima waende kunakohusika ambako vinatolewa vyeti vya Bakwata na Rita," anasema.
Anasema, kadhi wa kufungisha ndoa ana leseni ya Baraza (Bakwata) na kadi maalumu inayotambuliwa na Rita.
Naye Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini anasema si kila kiongozi wa Kikristo ana uhalali wa kufungisha ndoa.
"Ili ufungishe ndoa, lazima uwe na leseni ya Rita, wapo ambao hawana na wanafanya hivyo, ndoa hiyo inakuwa si halali kisheria hata kama imefungwa kwenye nyumba ya ibada.
"Na kiongozi aliyefungisha akibainika anachukuliwa hatua kisheria kwa kuwa ni kosa," anasema Askofu Kilaini.
Anasema unapofunga ndoa kwa imani ya Kikristo, wanandoa hupatiwa cheti cha Serikali kutoka Rita na kanisa huweka kwenye kumbukumbu zake kwamba ulifunga ndoa.
"Cheti hicho kinatolewa na kiongozi mwenye uhalali wa kufungisha ndoa tu, anayetambulika na Rita, kama hatambuliki hiyo ndoa itakosa uhalali,” anasema Kilaini.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni, Kimaro alisema cheti cha ndoa cha dini hakitoshi kukupa uhalali wa kisheria kuwa ni mke au mume.
Alisema, cheti hicho kitakutambulisha katika misingi ya dini, lakini inapofika kwenye sheria, hakiwezi kumtambulisha mhusika kwamba ni mke au mume halali.
"Unapofunga ndoa unapaswa kupewa cheti cha Serikali, na hiki kinatolewa na kiongozi wa dini mwenye leseni ya kufungisha ndoa, sio kanisa. Leseni hizi zinatolewa kwa mtu, kama ni mchungaji au shehe kwa jina na namba yake, siyo kwa kanisa au msikiti wake," alisema.
Kimaro alisema wanakutana na kesi nyingi za watu kufungishwa ndoa zisizotambuliwa na Rita.
"Wapo viongozi wa dini hawana leseni lakini wanafungisha ndoa, hii si sawa. Kabla hamjafunga ndoa, mnapaswa kumuuliza anayewafungisha kama ana leseni na kibali cha Rita cha kufungisha ndoa,” alisema.
Alisema yawezekana msikiti au kanisa lake limemuidhinisha kwa taratibu za dini yake, lakini ili aweze kufungisha ndoa lazima awe na cheti na leseni ya Serikali, kinyume na hapo haruhusiwi kufungisha ndoa.
"Kiongozi huyu akikufungisha ndoa na kukupa cheti, utakapofika kwenye masuala ya kisheria cheti hicho hakiwezi kukutambulisha kama mke au mume ili upate stahiki zako.
Hilo linathibitisha kilichomtokea Anitha John (si jina halisi) ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi, aliyeomba kumfuata mumewe mkoani Morogoro akakwama.
Anitha alifunga ndoa mwaka 2005, kwenye moja ya Kanisa Mwenge, jijini Dar es Salaam, kisha alipewa cheti cha dini na hakuwahi kubaini kwamba ndoa yake haijasajiliwa Rita, hadi alipoomba kumfuata mumewe.
"Tulipofunga ndoa tulipewa cheti kimoja, wasimamizi wetu wakaambiwa cheti kingine wakachukue makao makuu ya kanisa (anataja dhehebu).
Anasema ndoa yao ilifungwa Jumamosi huku mumewe akitakiwa kusafiri kwenda masomoni Ufaransa kwa miaka miwili.
"Mume wangu aliondoka baada ya ndoa, wale wasimamizi wetu walikifuata kile cheti na kuniletea kikiwa kimesainiwa na mchungaji na wao, mimi pia nilikisaini na kukihifadhi hadi mume wangu aliporudi naye akasaini.
'Kipindi chote hicho sikuwahi kujua kama hakitambuliki Rita hadi nilipokuwa nikifuatilia uhamisho," anasema.
Akifafanua hilo, Kimaro anasema hizo ni miongoni mwa changamoto nyingi za ndoa wanazozipokea katika ofisi hiyo.
"Pamoja na ndoa hizo kufungwa makanisani au misikitini, wanapofika Rita huwa hazitambuliki," anasema.
Anasema mara nyingi Rita hutoa elimu kwa jamii kuhakikisha wanapofunga ndoa ya dini, wanandoa wahakikishe wanapewa cheti cha Serikali.
Anasema kwa wale wanaofunga ndoa kanisani au msikitini na kupewa vyeti vya Serikali moja kwa moja, hao hawa hawana haja ya kwenda kusajili tena kwa kuwa cheti hicho tayari kimesajiliwa.
"Ambacho kinafanyika, hawa watasaini vyeti vitatu, kimoja ni cha mke, kingine cha mume na kingine kinabaki kwa yule aliyewafungisha ndoa, ambaye anakirudisha Rita," anasema.
Anasema wapo viongozi wa dini hawatoi vyeti vya Serikali, akitolea mfano ndoa za Kiislamu.
"Ukiwa na cheti cha Bakwata pekee, ndoa hiyo haitakuwa kwenye mfumo wa Rita na itakosa uhalali wa kisheria,” anasema Kimaro.
Wakili kiongozi wa kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza, Aloyce Komba anasema hata ndoa zinazofungwa nje ya nchi, lakini wahusika kwa namna moja ama nyingine wanahusiana na Tanzania, lazima ndoa zao zisajiliwe Rita.
"Hata ukifunga ndoa nje ya nchi, kama ni Mtanzania na unataka ndoa yako itambulike kisheria, unakwenda kuifunga kwenye ubalozi wa nchi yako katika nchi uliyopo au unakwenda kuisajili huko baada ya kufunga kidini," anasema