Rubani Gubuyi aendelea kusakwa
Rubani Samweli Gibuyi
Muktasari:
Vikosi vya uokoaji vyaingia katika misitu karibu na Mto Mtetesi
Dar es Salaam. Rubani Samweli Gibuyi wa ndege ya shirika la Pams Foundation aliyedaiwa kutoweka baada ya kuruka na ndege hiyo bado hajapatikana ikiwa leo ni siku ya 18 tangu kutokea kwa tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro ilisema Rubani huyo anadaiwa kupotea tangu Oktoba 18, mwaka huu majira ya saa tisa na dakika tisa jioni, alipokuwa akielekea usawa wa pori la akiba la Selous kanda ya Kingipira.
Akizungumza na Mwananchi jana Mtatiro alisema kwa sasa vikosi vinavyoshughulika na utafutaji vimewekeza nguvu kubwa katika misitu iliyopo karibu na mto Mtetesi ambako ambako wamekuwa wakipokea taarifa zinazoleta matumaini.
“Kutokana na taarifa hizo tumewekeza nguvu kubwa katika eneo hilo kwa kuwa eneo hilo la mto pia linazungukwa na misitu mikubwa hivyo tumevitawanya vikosi hivyo katika pande zote mbili zinazozunguunga mto huo,”alisema.
Pia Meneja wa mradi wa Pams, Max Jenes alisema za kumtafuta bado zinaendelea na wamekuwa wakiendelea kupokea taarifa kutoka kwa wananchi wanaodai kuiona ndege hiyo wakati ndege hiyo ikitokomea katika msitu .
“Tulisitisha utafutaji kwa kutumia ndege na hadi sasa tuna vikosi viwili ambavyo vinaendelea na utaftaji ardhini, vilevile wananchi walio karibu na hifadhi ambao walifanikiwa kuiona ndege hiyo wamekuwa wakiendelea kutupatia taarifa mbalimbali ,”alisema.
Naye Mdogo wa rubani huyo alisema Savatory Gibuyi alisema wao kama familia wanaiachia mamlaka husika inayofanya kazi hiyo huku wakiendelea kufuatilia taarifa kutoka katika mamlaka.
“Kuna vikosi mbalimbali vinavyofanya jitihada za kumtafuta ikiwemo wanaomtafuta kwa miguu, tunaiachia mamlaka huku tukiendelea kufuatilia taarifa za tukio hilo kwa ukaribu,“alisema.
Kwa nini ndege zinatoweka?
Aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihura alipofanya mahojiano na Mwananchi mwaka 2014 alisema sababu kubwa ya matukio hayo ni mabadiliko ya hali ya hewa na kuharibika kwa miundombinu, mambo ambayo husababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani.
“Matukio mengi kama haya ni kuwa ndege hugonga milima na kuanguka. Zikianguka sehemu za milima ni vigumu kupatikana kwa sababu wakati mwingine huganda katika barafu au kuzama kwenye makorongo,” alisema.
Alisema hata ndege zinazoanguka kwenye maji, pia ni vigumu kuonekana kutokana na kina kirefu au barafu.
Mtaalamu huyo alisema kuna baadhi ya ndege ambazo hupotea kutokana na rubani kukata mawasiliano kwa makusudi kwa sababu ama za kigaidi au magendo.
Alitoa mfano wa tukio la mwaka 1945, wakati ndege iliyokuwa ikitoka Malawi kwenda Nairobi, ilipopoteza mawasiliano ikiwa katika anga la Tanzania. Baadaye ilibainika kuwa rubani alifanya hivyo kwa makusudi ili ashushe bidhaa za magendo alizokuwa amepakia.
Sheria za anga za Tanzania zinakataza rubani kukata mawasiliano kwa makusudi na adhabu yake ni kufungiwa kabisa shughuli za urubani.
Matukio ya ndege kutoweka ulimwenguni
Amelia Earhart - 1937
Rubani wa Kimarekani, Amelia Earhart alikuwa mwanamke wa kwanza kuvuka Bahari ya Atlantic kuchunguza dunia, alipotea na ndege yake miongo saba iliyopita. Inahisiwa kuwa ndege yake iliishiwa mafuta na kuanguka.
Airbus A330 - 2009
Mwaka 2009 ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa, Airbus A330 iliyokuwa na abiria 228 ikitoka Rio de Janeiro, Brazil kwenda Paris, ilipotea kwa siku tano. Ilipatikana ikiwa imeanguka na kuungua. Hadi sasa maiti za abiria 74 bado hazijatambulika.
Flying Tiger 739 - 1962
Mwaka 1962 ndege ya kijeshi ya Marekani ilipotea ikiwa na watu 90 waliokuwa wanakwenda Ufilipino. Rubani wa ndege hiyo hakuwahi kutoa taarifa yoyote ya dharura na hadi sasa haijaonekana licha ya wataalamu 1,300 kushiriki kuitafuta.
South American Airways - 1947
Ilichukua miaka 50 kupata fununu za ndege ya Amerika ya Kusini iliyopotea mwaka 1947 ikiwa na abiria 11 na kupatikana mwaka 1998 katika Milima ya Andes. Ndege hiyo ilifunikwa kwenye barafu ya milima hiyo.
Bermuda Triangle - 1948 na 1949
Ulikuwa ni mfuatano wa matukio ya kupotea kwa ndege mbili katika eneo la baharini linaloitwa Pembetatu ya Shetani (Devil’s Triangle) katika maeneo ya Florida, Puerto Rico na Bermuda ambalo limekuwa na matukio mengi ya kupotea kwa ndege na meli kimiujiza. Katika matukio hayo mawili, ndege hizo zikiwa na jumla ya abiria 51 zilipotea na hata wanaanga 13 waliotumwa kuitafuta pia walipotea.
Uruguay 571- 1972
Ndege ya Shirika la Ndege la Uruguay, 571, ilipotea mwaka 1972 ikielekea Santiago, Chile. Ndege hiyo ambayo ilikuwa na abiria 45, ilianguka milimani na watu 12 walikufa. Walionusurika walitafutwa kwa zaidi ya siku 72. Kabla ya kuokolewa, majeruhi hao walilazimika kula nyama za wenzao waliokufa ili kuishi.