Saba kizimbani tuhuma wizi vyuma vya SGR

Friday November 27 2020
chumapic
By Mwandishi Wetu

Pwani.  Watu saba wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kibaha leo Ijumaa Novemba 27, 2020 kwa tuhuma za wizi wa vyuma vya reli ya kisasa (SGR).

Akizungumza leo mkurugenzi wa makosa ya jinai (DCI), Robert Boaz amesema wameshtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi, kwamba miongoni mwao wapo mawakala na  wafanyabiashara wa viwanda vya kuchakata vyuma chakavu.

Amebainisha kuwa Novemba 24, 2020 polisi walikamata watu watatu wilayani Kibaha wakisafirisha vyuma chakavu vikiwemo vyuma vilivyoibwa katika ujenzi wa reli hiyo mkoani Morogoro.

Boaz amesema baada ya uchunguzi wamefanikiwa kuwakamata wengine wanne na idadi kufikia watu saba ambao wamefikishwa mahakamani.

Amesema waliofikishwa mahakamani ni Luo Xingqui, Rospick Kimaro, Satyam Gupta,Florence Angelo,Halid Juma, Shadrack Makulu na Shakanyi Gambarata

"Serikali yetu inatumia pesa nyingi kuimarisha miundombinu ikiwemo reli lakini baadhi ya watu wasio wema na wenye uchu wa mali wamekuwa wakihujumu jitihada hizo hali hii haikubaliki,” amesema Boaz.

AdvertisementAdvertisement