Sababu Silinde kumsimamisha kazi mkuu wa shule

Tuesday February 23 2021
silinde pic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Naibu Waziri Tamisemi, David Silinde amemsimamisha kazi mkuu wa shule ya sekondari ya Kitama wilayani Tandahimba, Twaha Chitipu kwa  kushindwa kusimamia ujenzi wa bweni moja na matumizi mabaya fedha. 

Pia, amemtaka ofisa elimu wa sekondari wa Wilaya hiyo,  Sosteneth Luhende kuandika barua kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu na kuvuliwa madaraka baada ya kushindwa kusimamia  ujenzi wa mradi huo kwa ufanisi.

Silinde ametoa uamuzi huo jana Jumatatu Februari 22, 2021 alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa bweni hilo linalojengwa kwa Sh78milioni  huku akielezea masikitiko yake kwa namna ulivyojengwa chini ya kiwango.

“Maeneo mengine magumu yamemaliza ujenzi lakini ukija hapa ambapo Sh79 milioni zimelala hakuna kitu kilichofanyika. Hivi unajua mmeweka nondo za inchi tatu badala ya nne kwenye hili jengo?” 

“Nina hizo taarifa sikuja hapa kwa bahati mbaya, nilishasema nikienda sehemu siendi kwa kubahatisha. Naenda kukiwa na taarifa kwa sababu kuna mizaha mingi inafanyika,” amesema Silinde.

Katika maelezo yake, Silinde amesema ametembelea halmashauri ya Longido  na kukuta wamemaliza ujenzi wa  mabweni manne kwa Sh320 milioni ambapo kila bweni moja lilijengwa kwa Sh80 milioni.

Advertisement

“Kila kitu kimekamilika  ikiwemo miundombinu ya maji, kule ni mbali tofauti na hapa ambapo vitu ni bei nafuu lakini cha ajabu hapa mmenunua vitu gharama ya juu bila kubana matumizi angalia tu hata ujenzi wenyewe unatia mashaka,” amesema Silinde

Katika hatua nyingine, Silinde ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani humo kuanza uchunguzi mara moja utakaohusisha  mwenendo wa ujenzi wa jengo hilo na kumpa orodha ya bei ya kila kitu kilichotumika katika mchakato huo.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba , Sebastian Waryuba amesema wamepokea maelekezo  na maagizo na kwamba ataiagiza Takukuru kuanza  uchunguzi kuhusu mchakato huo.

Naye  Chitipu amesema miongoni mwa changamoto waliyopata wakati wa utekelezwaji wa mradi wa bweni hilo hadi kuchelewa kukamilika ilikuwa ni upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli za ujenzi.

Advertisement