SADC ilivyobadilisha Dar es Salaam
Muktasari:
- Wakati Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ukifanyika kuanzia kesho Jumamosi fahamu mambo yaliyolibadili jiji maarufu nchini Tanzania.
Dar es Salaam. Wanasema mgeni njoo mwenyeji apone suala hilo sasa limedhihirika jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wakati Mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiendelea mambo mengi yamebadilika ikiwemo usafi wa mwili na mazingira.
Vitu vingine ni kuwekwa taa mithili ya miti ya Krismasi barabarani pamoja na kuzuia kupiga picha katikati ya jiji hasa karibu na ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) unakofanyika mikutano hiyo.
Mkutano huo unaoshirikisha nchi 16 za SADC unafanyika kuanzia kesho Jumamosi jijini Dar es Salaam ambapo Mwenyekiti wa mkutano huo ni Rais John Magufuli wa Tanzania.
Mwananchi ilipita katika baadhi ya maeneo ndani ya jiji hili kuangalia hali ilivyo huku ikijaribu kuthibitisha kama kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyoitoa Julai 29, 2019 ya kuhamasisha usafi wa mazingira na mwili inatekelezwa.
Detricia Pamba, mkazi wa Jijini Dar es Salaam amesema tangu kutamkwa kwa kauli hiyo kwa sasa imekuwa mazoea kwamba hawezi kutoka bila kuwa safi.
Kuwekwa taa katika barabara ya Sam Nujoma kumewavutia wengi jambo ambalo linawafanya kushindwa kujizuia kupiga picha kutokana na mwonekano wake ambao haukuwepo awali.
Kuwekwa kwa taa hizo kunafanya kuwa eneo la pili linalovutia wakati wa usiku ikiwa ni baada ya daraja la Mwalimu Nyerere kuwa na taa zinazowaka nyakati za usiku katika eneo la katikati.
Pia, kutokana na mkutano huo, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imepiga marufuku pikipiki maarufu bodaboda kuingia katikati ya Jiji hali iliyozidisha madhara na kupunguza purukushani zilizokuwa zikitokana na bodaboda hizo.
Lakini kuzuia kupigwa picha katika eneo la Posta ni moja ya vitu ambavyo wengi hawajui hivyo ni vyema kuchukua tahadhari.