Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika, Zanzibar katika namba

Dar es Salaam. Leo Aprili 26, 2026, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaadhimisha safari ya kipekee ya miaka 62 tangu mataifa mawili huruTanganyika na Zanzibar yalipoamua kuungana na kuunda dola moja.

Muungano huu, uliowekwa rasmi kupitia makubaliano ya Aprili 22, 1964 na kuridhiwa Aprili 26, 1964 chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere na Abeid Amani Karume, umeendelea kuwa miongoni mwa miungano iliyodumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Katika kipindi chote, Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ripoti za Serikali na taasisi za kimataifa zinaonesha kwa uwazi safari ya Taifa hili kutoka misingi ya kisiasa hadi mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, pamoja na matarajio ya baadaye kuelekea mwaka 2050.


Mambo ya Muungano

Msingi wa Muungano huu ulijengwa kupitia Hati za Muungano za mwaka 1964, ambazo awali ziliainisha mambo 11 ya Muungano yaliyokabidhiwa Serikali ya Muungano. Mambo hayo yalihusisha maeneo nyeti kama Katiba, mambo ya nje, ulinzi, polisi, uraia, uhamiaji, fedha na biashara ya nje.

Hata hivyo, kadri Taifa lilivyokua, orodha hiyo ilipanuka na kufikia mambo 22 kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Ongezeko hili lilitokana na mahitaji mapya ya kiuchumi na kisiasa, likijumuisha sekta kama sarafu na benki, elimu ya juu, mafuta na gesi, pamoja na usajili wa vyama vya siasa.

Mabadiliko haya hufanyika kwa utaratibu maalumu unaohitaji theluthi mbili ya wabunge kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar, jambo linaloonyesha uzito wa kulinda usawa ndani ya Muungano.


Idadi ya watu, makazi

Kwa mtazamo wa idadi ya watu, takwimu zinaonyesha ukuaji mkubwa wa Taifa hili. Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 1967, Tanzania ilikuwa na watu milioni 12.3 pekee.

Lakini, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 iliyotolewa na NBS, idadi hiyo imeongezeka hadi watu milioni 61.74. Kati ya hao, Tanzania Bara ina watu milioni 59.85 huku Zanzibar ikiwa na watu milioni 1.89.

Hii ina maana kuwa ndani ya kipindi cha miaka 55, idadi ya watu imeongezeka zaidi ya mara tano.

Aidha, kasi ya ukuaji wa watu imeongezeka kutoka asilimia 2.7 kati ya 2002 na 2012 hadi asilimia 3.2 kwa mwaka kati ya 2012 na 2022, hali inayoendelea kuweka shinikizo kwa huduma za kijamii na rasilimali.

Vile vile Ripoti ya “Population Dynamics” ya NBS inaonesha kuwa idadi ya watu inaweza kufikia milioni 118 ifikapo mwaka 2050.

Sambamba na ongezeko hilo la watu, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya makazi. Mwaka 1967, ni asilimia 5.7 tu ya Watanzania waliokuwa wanaishi mijini. Lakini, kufikia mwaka 2022, asilimia 34.9 ya watu wanaishi katika maeneo ya mijini.

Zanzibar imeonesha kasi kubwa zaidi ya ukuaji wa mijini, ambapo asilimia 49 ya wakazi wake sasa wanaishi mijini. Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa idadi ya watu, ukiwa na zaidi ya watu milioni 5.3, sawa na karibu asilimia 9 ya Watanzania wote.

Takwimu hizi zinaashiria kuwa ifikapo mwaka 2050, zaidi ya nusu ya Watanzania wataishi mijini, jambo litakalohitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu na huduma za kijamii.


Utawala, demokrasia na uchumi

Katika nyanja ya utawala na demokrasia, Muungano umeendelea kuimarika kwa kuzingatia uwakilishi.

Katika kipindi cha 1967 hadi 1970, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya kazi chini ya Katiba ya muda ya 1964, likiwa na muundo wa uwakilishi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Japo hakuna takwimu rasmi za wawakilishi wakati wa Muungano, uchaguzi wa 1970 ulionyesha jumla ya wabunge 237.

Kati yao, Tanzania Bara ilikuwa na takriban wabunge 159, wakiwemo wa majimbo, walioteuliwa na Rais na wajumbe wa nafasi za kiofisi. Zanzibar ilikuwa na takriban wabunge 67, wengi wao wakitoka Baraza la Mapinduzi na uteuzi wa Rais wa Zanzibar. Mfumo huo uliipa Zanzibar uwakilishi maalum ili kulinda mizania ya kisiasa ndani ya Muungano.

Kwa sasa, Bunge la Jamhuri ya Muungano lina jumla ya viti 393 kwa mujibu wa takwimu za uchaguzi wa mwaka 2025, ambapo majimbo ya uchaguzi yalikuwa 264.

Kati ya hayo 214 kutoka Tanzania Bara na 50 kutoka Zanzibar. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024/25, wabunge wanawake ni 148 kati ya wabunge 392, sawa na asilimia 37.8.

Hii inaonyesha kuwa Tanzania imevuka kiwango cha chini cha asilimia 30 cha uwakilishi wa wanawake, hatua inayotafsiriwa kama mafanikio ya sera za usawa wa kijinsia.

Kiuchumi, Muungano umewezesha uwepo wa soko moja na mfumo wa sarafu moja. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianzishwa mwaka 1965 na kuanza kazi rasmi mwaka 1966, ikichukua nafasi ya mfumo wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.

Mfumo huu umehakikisha uthabiti wa fedha na kurahisisha shughuli za kiuchumi kati ya pande mbili za Muungano. Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, Pato la Taifa lilifikia takriban dola za Marekani bilioni 60.5 (Sh151.3 trilioni) mwaka 2021, huku sekta mbalimbali kama utalii, kilimo na huduma zikichangia kwa kiasi kikubwa.

Takwimu pia zinaonyesha ukuaji wa sekta zisizo za kiserikali. Kufikia mwaka 2022, Tanzania ilikuwa na zaidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali 17,500, ambayo yamekuwa yakichangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kushirikiana na Serikali.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya, takwimu zinaonyesha changamoto zinazoibuka kadri Taifa linavyokua. Ripoti ya “Population Dynamics” ya NBS inaonesha kuwa idadi ya watu inaweza kufikia milioni 118 ifikapo mwaka 2050.

Ongezeko hili lina maana kubwa kwa sekta muhimu. Katika afya, mahitaji ya zahanati yanatarajiwa kuongezeka kutoka 7,734 mwaka 2022 hadi zaidi ya 26,500 mwaka 2050, huku mahitaji ya wauguzi yakiongezeka zaidi ya mara mbili.

Gharama za uendeshaji wa sekta ya afya zinatarajiwa kupanda kutoka Sh7.2 trilioni hadi zaidi ya Sh36 trilioni kwa mwaka.

Katika elimu, mahitaji ya walimu yataongezeka kwa kasi kubwa. Walimu wa shule za msingi wanatarajiwa kuongezeka kutoka 175,687 hadi zaidi ya 341,000 ifikapo 2050, wakati walimu wa sekondari wataongezeka hadi zaidi ya 200,000. Hii ina maana kuwa uwekezaji mkubwa unahitajika ili kukidhi mahitaji ya kizazi kijacho.

Katika sekta ya ardhi na kilimo, changamoto inaonekana zaidi kupitia mgawanyo wa rasilimali. Mwaka 2022, wastani wa ardhi inayolimika kwa kila mtu ulikuwa hekta 0.70, lakini unatarajiwa kushuka hadi hekta 0.37 ifikapo mwaka 2050 kutokana na ongezeko la watu.

Wakati huo huo, uzalishaji wa mazao unapaswa kuongezeka karibu mara mbili ili kukidhi mahitaji ya chakula.