Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari ya Wamwera kutoka Lindi hadi Dar kumuaga Membe

Baadhi ya waombolezaji katika hafla ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee

Muktasari:

  • Kilometa 460.3 hazikuwa tatizo kwa wananchi wa Jimbo la Mtama, kabila la Wamwera kufunga safari kutoka Lindi hadi Dar es Salaam kutoa heshima katika hafla ya kitaifa ya kumuaga Bernard Membe.

Dar es Salaam. Imezoeleka tamaduni za makabila mengi nchini kushiriki matukio ya msiba wa ndugu, jamaa au jirani yao, utamaduni huu umedhihirishwa na wazee wa kabila la wamwera waliofunga safari kutoka Rondo mkoani Lindi hadi jijini hapa ili kutoa heshima ya mwisho kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Katika mahojiano na Mwananchi Digital viwanja vya Karimjee jijini hapa ambapo hafla hiyo ya kitaifa inafanyika leo Jumapili ya Mei 14, 2023 mmoja wa wazee hao, Abdallah Hassan amesema alifunga safari juzi kutoka Lindi kuja Dar es Salaam japokuwa hawakuwahi kuonana ana kwa ana wakati wa uhai wake.

"Huyu aliyefariki ni mmwera na mimi ni mmwera kwa hiyo ni ndugu yangu nimekuja kwenye msiba wa ndugu yangu, siko peke yangu tulikodi gari (Coaster) kuja katika msiba huu," amesema.

Ameeleza ni desturi ya watu wa kabila hilo, kushiriki kikamilifu kwenye matukio yanayomhusu yeyote mwenye asili ya kwao.

"Wengine wanaofariki ni vile tu huwa hatuna taarifa, lakini msiba huu wa kitaifa tumepata taarifa tupo wengi tuliokuja kushiriki shughuli mbalimbali," amesema.

Mwingine katika msafara huo ni Nasimu Mpache ambaye amesema amelazimika kufanya safari hiyo kutokana na undugu wake na Membe kwa mujibu wa taratibu za kabila lao.

"Membe ni Mmwera nami ni wa kabila hilo ni ndugu yangu, tukitoka hapa tunasafiri na mwili hadi nyumbani kwa ajili ya mazishi," amesema.

Amesema pamoja na ushiriki wake Dar es Salaam, wapo walioachwa Rondo kwa taratibu nyingine za maandalizi ya kupokea wageni na nyinginezo ili kuratibu maziko.

"Asili yetu sisi kila mmwera ni ndugu yako wa damu huwezi kumuacha ateseke au kwenye shida huwa tunashirikiana," ameeleza Nasimu.

Nasimu aliongozana na wenzie takriban 15 anaoeleza walikuwa sehemu ya msafara kutoka Lindi hadi Dar es Salaam amesema Membe alisaidia kuleta maendeleo katika Jimbo lake akiwa mbunge.

"Alitufanyia makubwa sana Mtama, tulikuwa kama tumesahaulika lakini huyu mzee (Membe) akiwa Mbunge tulineemeka kwa kweli," amesema.